Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imesema imepokea taarifa za kutisha kuwa waasi wa RSF wanafanya ukatili wa kutisha nchini Sudan.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema RSF hivi karibuni imechukua sehemu kubwa eneo la El Fasher katika jimbo la Darfur Kaskazini na jiji la Bara katika jimbo la Kordofan Kaskazini, jambo ambalo limeongeza hofu ya mateso makubwa kwa raia.

Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema: “Katika eneo la El Fasher, taarifa za awali zinaonesha hali hatarishi sana tangu RSF ilipotangaza wameshika udhibiti wa kikosi cha 6 cha askari wa miguu.” 

Ameongeza kuwa:“Hali ya kuongezeka kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaochochewa na ubaguzi wa kikabila katika mji wa El Fasher inazidi kuongezeka kila siku. Hatua za dharura zinahitajika ili kulinda raia.”

Ameongeza kuwa ” Video za kusikitisha zinaonesha wanaume wengi wasio na silaha wakiuawa au wakiwa wamezama kwenye maiti, wakidaiwa kuwa wanajeshi wa Jeshi la Sudan”.

Mauaji ya kikatili pia yameripotiwa katika jiji la Bara, Kordofan Kaskazini, kufuatia kushikiliwa kwake na RSF tarehe 25 Oktoba.

Waathirika walidaiwa kuwa wanasiasa au wafuasi wa Jeshi la Sudan. “RSF lazima ichukue hatua za dharura kumaliza na kuzuia ukatili dhidi ya raia katika mji wa El Fasher na Bara,” amesema Türk, akisisitiza kuwa sheria za kibinadamu za kimataifa zinakataza ukatili dhidi ya wale wasiokuwa sehemu ya mapigano.

Türk amezitaka nchi wanachama zenye ushawishi kwa RSF kuchukua hatua mara moja ili kuzuia utekaji wa mateso zaidi.

Amemalizia kwa kusema kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali hii, akisisitiza umuhimu wa kufikisha msaada wa kibinadamu na kulinda raia.

Jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023, vita ambavyo tayari vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na kupelekea zaidi ya watu milioni 14 kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi. Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, kuwa ni muungaji mkono mkuu wa waasi wa RSF, tuhuma ambazo wakuu wa nchi hiyo ya Kiarabu wamekanusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *