Dar es Salaam. Kutotumika kwa Uwanja wa Azam Complex katika hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, kumeifanya Singida Black Stars kuamua kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar kwa mechi za hatua hiyo zitakazoanza mwezi ujao.

Singida Black Stars ilitumia Uwanja wa Azam Complex katika mechi za hatua ya awali lakini kwa mujibu wa mahitaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ya viwanja vya kutumika kwa hatua ya makundi na zile za juu za mashindano hayo, uwanja huo hauruhusiwi kutumika.

“Uwanja unatakiwa angalau uwe na uwezo wa kuwa na siti 10,000,” inafafanua Ibara ya 4(2)(i) ya muongozo wa mahitaji ya CAF ya viwanja kwa hatua ya makundi au zaidi.

Taarifa iliyotolewa na Singida Black Stars leo, imeeleza kwamba timu hiyo mechi zake zitachezwa Zanzibar.

“Tumechagua kuutumia Uwanja wa New Amaan-Zanzibar kama uwanja wa nyumbani kwenye mechi zetu za Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).

“Uamuzi huu umefikiwa kwa kuzingatia ubora wa miundombinu ya uwanja huo, mazingira rafiki, uzoefu wetu na uwanja na urahisi wa maandalizi.

“Tunawaalika mashabiki wetu wote wa Tanzania Bara na Visiwani kuungana nasi kwa nguvu zote katika safari nyingine ya kihistoria itakayoanza Novemba, 2025,” imefafanua taarifa ya Singida Black Stars.

Hii ni mara ya kwanza kwa Singida Black Stars kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mashindano ambayo inashiriki pia kwa mara ya kwanza.

Singida Black Stars imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuzitupa nje timu za Rayon Sports ya Rwanda na Flambeau Du Centre ya Burundi katika raundi mbili za awali za mashindano hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *