
Klabu ya Singida Black Stars, imeuchagua Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kuwa uwanja wake wa nyumbani kwenye mashindano ya kimataifa, huku ikitaja sababu tatu za kufanya hivyo.
Singida Black Stars ipo hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo imefuzu baada ya kuifunga Flambeau du Centre ya Burundi kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Singida Black Stars imeeleza sababu ya kuchagua uwanja huo kuwa ni uwepo wa miundombinu bora, urahisi wa maandalizi na uzoefu wa klabu uliyonayo kwenye uwanja huo.
“Tumechagua kuutumia Uwanja wa New Amaan-Zanzibar kama uwanja wa nyumbani kwenye mechi zetu za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
“Uamuzi huu umefikiwa kwa kuzingatia ubora wa miundombinu ya uwanja huo, mazingira rafiki, uzoefu wetu na uwanja na urahisi wa maandalizi,” imeeleza taarifa hiyo.
Kabla ya kuhamia New Amaan Complex, timu hiyo ilikuwa ikiutumia Uwanja wa Azam Complex uliopo Dar es Salaam kwenye hatua za mtoano za mashindano hayo ambapo ilicheza mechi mbili dhidi ya Rayon Sports na Flambeau ambazo zote imeshinda.
Hata hivyo, klabu hiyo imewaomba mashabiki ushirikiano katika kipindi itakapokuwa ikicheza mechi zake huko.
“Tunawaalika mashabiki wetu wote wa Tanzania Bara na Visiwani kuungana nasi kwa nguvu zote katika safari nyingine ya kihistoria itakayoanza Novemba 2025,” imebainisha taarifa hiyo.
Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi mbili zilizofanikisha kuingiza timu nne katika hatua ya makundi ya mashindano ya CAF ngazi ya klabu msimu huu sambamba na Algeria.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Singida Black Stars ipo na Azam, huku Yanga na Simba zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.