
Jenerali al-Burhan amekiri siku ya Jumatatu kwamba jeshi “limejiondoa” katia mji wa El-Fasher, ngome yake ya mwisho magharibi mwa nchi.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Pamoja na mwandishi wetu wa kikanda, Gaëlle Laleix
Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, amekiri Jumatatu, Oktoba 27, kwamba “jeshi limejiondoa katika mji wa El Fasher” siku moja baada ya Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, kutangaza kuliteka jiji hilo. RSF imekuwa ikipigana na jeshi la Jenerali Abdel Fattah al-Burhan tangu mwezi Aprili 2023.
“Tumekubali kujiondoa kwa jeshi kutoka El Fasher hadi mahali salama zaidi,” Jenerali al-Burhan ametangaza katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni ya kitaifa, akithibitisha kwamba upande wake “utalipiza kisasi” na kupigana “hadi tutakaposafisha ardhi hii.”
Siku ya Jumapili, Oktoba 26, katika taarifa kwenye mtandao wa ujumbe wa Telegram, wanamgambo wa RSF wa Jenerali Hemedti walidai kuuteka mji wa El-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini. Ulikuwa umezingirwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka kwa miezi 18. Umoja wa Mataifa unaonya kuhusu “ukatili” unaochochewa kikabila, na Antonio Guterres anatoa wito kwa nchi ambazo “hutoa silaha kwa pande zinazopigana ili kusitisha tabia hiyo.”
Tangu saa za mapema za Jumatatu, RSF imekuwa ikirusha video kwenye Telegram za wanajeshi wao wakipiga picha mbele ya makao makuu ya Kitengo cha 6 cha Jeshi la Wanamaji, ambacho kilitelekezwa na wanajeshi wake siku ya Jumapili. Kwenye mtandao wa kijamii wa X, gavana wa Darfur, aliyeteuliwa na Muungano wa Tasis—umoja unaotii RSF uliounda serikali sambamba na ile ya Port Sudan mwaka huu—amekaribisha “ukombozi wa El Fasher.”
Jeshi awali lilibaki kimya, kabla ya Jenerali al-Burhan kukiri kuanguka kwa El Fasher Jumatatu jioni. Waziri wa Habari alitoa taarifa siku ya Jumatatu asubuhi akisifu “azma” ya wanajeshi wa Sudan ambao waliendelea “kurudisha nyuma” shambulio la RSF dhidi ya El Fasher. Kamati za Upinzani wa Raia, kwa upande wao, zimehakikisha kwamba jiji halitakuwa chini ya amri ya wanamgambo wa RSF.
Gavana wa Darfur Kaskazini anatoa wito wa “ulinzi wa raia”
Kwa vyovyote vile, hali ya kibinadamu ina hatari ya kuzorota zaidi. Baada ya miezi 18 ya kuzingirwa katika hali kama ya njaa, wakazi wa El Fasher wanajikuta katikati ya mapigano. Mini Minawi, gavana wa Darfur askazini aliyeteuliwa na jeshianaomba kupitia ukurasa wake wa X “ulinzi wa raia,” jambo ambalo RSF imeahidi kusimamia katika taarifa yao ya hivi karibuni.
Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Solidarity International, malori manne ya RSF yalifika Jumapili jioni huko Tawila, kilomita 60 kutoka El-Fasher, yakiwa yamebeba kati ya watu 200 na 400. Watu hawa waliohamishwa wako katika hali mbaya; wana utapiamlo na wamepungukiwa na maji mwilini. Tangu mwezi Aprili, zaidi ya watu nusu milioni waliokimbia makazi yao waliwasili Tawila.
Umoja wa Mataifa unalaani “kuongezeka kwa mgogoro mbaya”
Hali ya kibinadamu huko Darfur inamtia wasiwasi mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye analaani “kuongezeka kwa mgogoro mbaya,” na wito wa kimataifa unaongezeka ili kuruhusu ufikiaji wa kibinadamu kwa raia wanaotaka kuondoka mji huo…
“Hii inawakilisha kuongezeka kwa mgogoro mbaya,” Antonio Guterres alijibu swali kutoka kwa shirika la habari la AFP wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia, siku ya Jumatatu.
Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi zinazosambaza silaha kwa pande zinazopigana kukomesha tabia hiyo: “Nadhani ni wakati mwafaka kwa jumuiya ya kimataifa kuweka wazi kwa nchi zote zinazoingilia vita hivi na kusambaza silaha kwa pande zinazopigana ili kukomesha. Kwa sababu kiwango cha mateso tunachokiona nchini Sudan hakiwezi kuvumilika,” amebainisha.
Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ametoa wito wa njia salama kwa raia huku njia za uokoaji zikikatizwa: “Mamia ya maelfu ya raia wamenaswa na kuogopa – wakishambuliwa kwa mabomu, wanakufa njaa, na hawana upatikanaji wa chakula, huduma ya afya, au usalama,” amesema. Kwa upande wao, Mtandao wa Madaktari wa Sudan kwa mara nyingine tena umelaani dhuluma zinazoathiri kikosi cha matibabu huko El Fasher.
“Hatari ya ukiukwaji mkubwa wa kikabila na ukatili”
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameonya siku ya Jumatatu kwamba jiji la El Fasher liko katika “hali mbaya sana,” huku akisema kuna mateso na hatari ya “ukiukwaji mkubwa kwa misingi ya kikabila .”
“Hatari ya ukiukwaji mkubwa haki kwa misingi ya kikabila na ukatili huko El-Fashir inaongezeka kila siku,” Bw. Türk amesema katika taarifa, akitaka “hatua za haraka na thabiti (…) ili kuhakikisha ulinzi wa raia huko El-Fashir na njia salama kwa wale wanaojaribu kufika maeneo salama.