
Tamko hilo limepitishwa na jumuiya hiyo yenye wanachama 10 mnamo tarehe 26 mwezi Oktoba, wakati wa Kikao cha 47 cha Kilele cha ASEAN kilichofanyika huko Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia.
“Tamko la ASEAN kuhusu Haki ya Mazingira Salama, Safi, Yenye Afya na Endelevu ni hatua muhimu sana, kwa kuwa ndilo tamko la kwanza la kikanda kuthibitisha haki ya kuwa na mazingira yenye afya katika eneo lote Kusini-Mashariki mwa Asia,” amesema Türk
Akitoa wito kwa nchi zote kuongeza juhudi katika kutekeleza haki ya mazingira yenye afya kwa wote amesema“Ni hatua ya pamoja yenye umuhimu mkubwa wakati huu ambapo changamoto nyingi za kimazingira, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na upotevu wa viumbehai, zinaongezeka duniani kote,”.
Kudumisha uongozi wa pamoja
Kamishna Mkuu amewahimiza Nchi Wanachama wa ASEAN kujenga juu ya msingi wa tamko hilo ili kuhakikisha uongozi wa pamoja na hatua za haraka katika kukabiliana na madhara ya mazingira yanayovuka mipaka, kama vile mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa ardhi, maji na hewa, kwa ushiriki wenye maana wa walioathirika zaidi, wakiwemo wanawake, vijana, na Watu wa Asili. Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ulinzi madhubuti kwa watetezi wa haki za binadamu za mazingira na kazi yao muhimu.
“Nchi wanachama wa ASEAN zinapaswa sasa kuchukua hatua za haraka kutafsiri ahadi zilizomo kwenye tamko hili kuwa sheria, sera na vitendo, ikiwemo hatua za kuwajibisha wahusika wa sekta binafsi kwa uharibifu wa mazingira. Muda ni muhimu, kwani madhara ya mazingira yanaongezeka na kuzidi kuwa makubwa,” amesema mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Tamko hili ni nyenzo ya hivi karibuni ya kikanda inayohusisha haki za binadamu na mazingira, ikifuatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 76/300 ambalo lilitambua haki ya kimataifa ya kuwa na mazingira safi, yenye afya na endelevu, pamoja na maoni ya ushauri ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu wajibu wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Türk amehakikishia ASEAN na nchi wanachama wake kuwa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ipo tayari kusaidia katika utekelezaji wa tamko hilo, ikiwemo kupitia ushirikiano wa kiufundi, ujenzi wa uwezo, na utayarishaji wa mpango wa kikanda wa utekelezaji.
Aidha, amezihimiza nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuendelea kusukuma mbele hatua za kimazingira zinazozingatia haki za binadamu, kwa kuendana na viwango vya kimataifa vinavyoendelea kubadilika haraka katika eneo hili.