Lakini umataifishaji au Internationalisation kwa kiingereza ni nini ? Umataifishaji ni mchakato wa kuingiza vipengele vya kimataifa katika majukumu ya msingi ya taasisi ya elimu, kama vile ufundishaji, utafiti, na huduma. Hatma ya umataifishaji ni lengo namba 4 la kuboresha elimu na wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kushindana kimataifa.

Ni katika muktadha huo, TANZANIA Internationalisation strategies for Higher Education, kwa kifupi TANZIE, mradi unaofanikishwa na Muungano wa Ulaya, EU, unalenga kukidhi mahitaji ya umataifishaji Tanzania, na Chuo Kikuu Mzumbe ni mmoja wa wadau.

Profesa William Mwegoha, Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe.

Profesa William Mwegoha, Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe.

Na ndipo Profesa Mwegoha anasema, “sasa ili kutoa elimu bora ni lazima tuwe tunaweza kunyanyua viwango, kuwa na mafunzo ya kutoa elimu bora. Ni muhimu sana na programu zake ziwe na uwezo wa kuwa na ubora wa kutosha sana kukidhi matakwa ya sio tu ya Tanzania, lakini pia ya eneo la Afrika Mashariki pia na ya kidunia.”

Profesa Mwegoha amesema hayo akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Morogoro baada ya kufunga mafunzo kwa wakufunzi ya Mradi wa Tanzania unaohusisha Vyuo Vikuu vya Tanzania na vya nchi za Muungano wa Ulaya, TANZIE, yaliyofanyika kwa siku tatu katika Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro.

Ubia wa Vyuo Vikuu vya Tanzania na Muungano wa Ulaya

Mkurugenzi wa Idara ya Umataifishaji ya Baraza la Wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lucy Massoi anabainisha malengo ya mradi wa TANZIE akisema, “umelenga katika kujenga mifumo imara na endelevu ya ukimataifishaji ambayo itaongeza ubora wa ufundishaji, utafiti na ushirikiano wa kitaaluma. Lakini kwa kipekee hasa mradi huu una malengo mahususi mawili. Lengo la kwanza ni kuimarisha uwezo wa taasisi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini shughuli za kimataifa na lengo la pili ni kukuza umahiri wa kiutamaduni na kimataifa miongoni mwa wafanyakazi na wanafunzi ili kuunda mazingira ya ujifunzaji yenye mtazamo wa dunia.”

Mradi wa TANZIE unafanyika kwa ubia baina ya Muungano wa Ulaya kupitia Vyuo Vikuu vya Alicante cha Hispania, Saarland cha Ujerumani na EFDM kutoka Ubelgiji pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe cha Morogoro, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo jijini Arusha, Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afya na Sayansi CUHAS Bugando, Mwanza, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.

Mwakilishi wa Muungano wa Ulaya na Mkufunzi Mkuu wa Mafunzo ya wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Alicante Hispania, Dkt. Mario Aguero katika mahojiano anasema wanayo furaha kuratibu mradi wa TANZIE na kwamba Muungano wa Ulaya umejizatiti kuunga mkono juhudi hizo.

Dr. Mario Guillo, Mkufunzi Mkuu wa Mradi wa TANZIE kutoka Chuo kikuu cha Alicante Hispania.

Dr. Mario Guillo, Mkufunzi Mkuu wa Mradi wa TANZIE kutoka Chuo kikuu cha Alicante Hispania.

Faida za umataifishaji

Dkt. Mario anasema, ”umataifishaji unaleta manufaa mengi. Unaleta fursa nyingi za uboreshaji elimu ya juu, utaleta mikakati sahihi ya umataifishaji, kufanikisha upatikanaji wa rasilimali, ujuzi, kuunganisha mtandao na Taasisi husika duniani kwa ajili ya kuimarisha sio tu ubora wa elimu lakini pia utafiti na kuhamisha maarifa.”

Kwa upande wa CUHAS Bugando, Mwanza, mradi wa TANZIE umesukuma kuanzisha kitengo cha utaifishaji, anasema Afisa Uhusiano Tandiwe Peter, akisema, “tutakwenda kuanzisha kitengo cha kitaasisi cha umataifishaji katika chuo chetu, lakini pia kuhakikisha kwamba zile shughuli ambazo zilikuwa zinafanyika katika umataifishaji chuoni zinafanyika kwa ufanisi zaidi na kujengea uwezo wadau wengine wa ndani wa chuo, lakini pia kuendelea kuboresha mahusiano na wadau wa nje ili kukuza zaidi utekelezaji wa Sera ya umataifishaji kitaifa na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *