Maeneo mbalimbali ya Cameroon yameendelea kushuhhudia maandamano ya watu wenye hasira wanaopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi rais kizee zaidi duniani yaani Paul Biya mwenye umri wa miaka 92.

Mji ulioshuhudia maandamano makubwa zaidi ni wa Douala ambako watu wamekuwa wakiandamana kwa siku ya pili mfululizo, kufuatia tangazo kwamba Rais Paul Biya amechaguliwa tena kwa muhula wa nane. Wanajeshi wametawanywa kwenye maeneo mbalimbali ya mji huo kukabiliana na maandamano ya fujo.

Vizuizi na milio ya risasi za moto imesikika huko Douala, kama ilivyo katika miji mingine mingi ya Cameroon. Yote hayo yametokea baada ya Rais Paul Biya kutangazwa tena kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Jana Jumatatu, Baraza la Katiba la Cameroon lilimtangaza Rais wa hivi sasa wa nchi hiyo Paul Biya kuwa msindi wa uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura na kumfungulia njia ya kuendelea kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa nane mfululizo. Paul Biya anahesabiwa kuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi na aliyekaa madaraka kwa muda mrefu zaidi. Amekuwa akiongoza Cameroon tangu mwaka 1982 bila ya kukatizwa. 

Tangazo la ushindi wa Paul Biya ambalo limepingwa na mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, limezusha hasira kubwa za wananchi wa Cameroon hasa wa mji wa Douala.

Mmoja wa wakazi wa mji wa Douala aliyejitambulisha kwa jina la Max Ndongmo amesema kuwa hasira hizo wanazo wananchi wengi wa Cameroon. Amesema Wacameroon wengi wamevunjika moyo waliposikia matokeo ya uchaguzi huo. “Mimi mwenyewe nitakwambia ukweli wangu, ilinishtua sana kiasi kwamba karibu nivunje TV yangu. Wanachofanya na ambacho wamekuwa wakifanya miaka yote hii, ni unafiki tu.”

Hali ya usalama katika mji wa Douala si shwari kiasi kwamba wanajeshi wamepelekwa kwenye wilaya kadhaa za mji huo. Uporaji, uharibifu wa maeneo ya umma na risasi za moja kwa moja zimetukia ikiwa ni kuashiria kuwa kazi zote za mji huo zimesimama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *