
Watanzania kesho watapiga kura katika uchaguzi mkuu wa kuwachagua madiwani, wabunge na Rais, huku kampeni zikimalizika leo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Rais Samia Suluhu Hassan, anapeperusha bendera ya chama tawala CCM, kwenye uchaguzi huu anaotarajiwa kushinda, kutokana na kile wachambuzi wa siasa wanasema hakabiliwi na upinzani mkali.
Mpinzani wake Mkuu Tundu Lissu, yupo jela kwa tuhuma za uhaini. Kule Visiwani Zanzibar, mgombea mkuu wa upinzani Othman Masoud Othman kutoka chama cha ACT Wazalendo, amesema hatarajii uchaguzi huo kuwa huru na haki.
‘‘Tumechambua daftari la wapiga kura ambalo limetangazwa na Tume ya uchaguzi, kuna watu kadhaa ambao ni wazi hawatakiwi kuwa wanachama wa CCM.’’ Alisema Othman Masoud Othman kutoka chama cha ACT Wazalendo
Katika hatua nyingine, rais Hussein Mwinyi mgombea wa chama tawala CCM akitamatisha kampeni zake, alisema ana uhakika wa kushinda uchaguzi huo wakati wa kampeni yake ya mwisho.
‘‘Hakuna sababu kwa nini chama cha mapinduzi kisishinde kwa ushindi mkubwa tarehe 29.’’ Alisema Mwinyi.
Haya yanajiri wakati huu, wapiga kura visiwani Zanzibar wakianza zoezi la kupiga kura la mapema hivi leo, kabla ya siku yenyewe ya upigaji kura hapo kesho.