Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi tayari amepiga kura katika kituo cha kupigia kura Kariakoo viwanja vya michezo ya watoto Jimbo la Kwahani.
Dk Mwinyi amefika katika kituo hicho saa 2:10 asubuhi ya leo Jumatano, Oktoba 29, 2025 akiwa ameongozana na familia yake, mke wake, Mariam na watoto wake watatu.
Baada ya kufika katika kituo hicho, alipanga foleni katika mistari ya wananchi ambao nao walikuwa kwenye foleni kwa ajili ya kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura, Dk Mwinyi anayetetea nafasi hiyo amesema ametimiza haki yake ya kikatiba na kwamba amefurahishwa kuona wananchi wamejitokeza kwa wingi kupiga kura.
“Nimetekeleza wajibu wangu kikatiba, nimeshapiga kura, tumeridhika na maandalizi yaliyofanywa na Tume kwakweli ni mazuri,” amesema Dk Mwinyi.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi ambao bado wapo nyumbani wajitokeze kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowatumikia kwa kipindi cha miaka mitano.
Pia, Dk Mwinyi amepongeza amani ambayo imetawala kuanzia wakati wa kampeni mpaka asubuhi hii saa mbili kwani hakuna viashiria vyovyoye ambavyo vinetokea kuashiria uvunjifu wa amani.
“Tumefanya kampeni kwa amani kabisa hatukuona chokochoko, mpaka sasa tunaona amani ipo ni imani yetu hali itaendelea hivi hata baada ya kutangazwa matokeo,” amesema Dk Mwinyi.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza wapinzani wake 11 anaoshindana nao kujitokeza kuwania nafasi hiyo akisema jambo hilo linaonesha kukuwa kwa demokrasia katika visiwa hivyo.
Hata hivyo, amesema kulingana na kampeni walizofanya wanaamini wanachi wamewakubali na watashinda katika uchaguzi huu.
Naye Mke wake, Mariam amesema:”Siku ya leo tulikuwa tunaisubiria sana tukisema Oktoba 29, imefika kwa hiyo wananchi tujitokeze kwa wingi kupiga kura. Shime shime tujitokeze kwa wingi kupiga kura,” amesema.