Dodoma. Hali ya utulivu imetawala katika Jiji la Dodoma na viunga vyake, watu ni wachache sokoni, magari ni machache barabarani huku maduka mengi yakionekana makufuli.

Hadi saa 3.45 asubuhi ya leo Jumatano, Oktoba 29, 2025 mji ulikuwa umepoa na maeneo machache Polisi walikuwa wakipita lakini maeneo ya katikatika ya mji (One Way) ambako huwa na msongamano wa watu kulikuwa na idadi ndogo ya watu.

Mtaa wa Uhindini unaopakana na soko la Sabasaba ambao unatajwa kuwa maarufu kwa migahawa ya vyakula, nako kulitulia na baadhi ya migahawa kufungwa.

Soko la Machinga ndiyo pekee lilionekana kuwa na pilikapilika lakini hata hivyo haikuwa kama ilivyozoeleka kwa mtazamo wa siku zote.

Wakati hali ikiwa hivyo, vituo vya kupigia kura katika Kata za Nzuguni, Makole, Ipagala na Viwanda hadi saa 2.50 asubuhi watu walionekana kujitokeza mapema kwa idadi ambayo baadhi ya watu wamesema inatia moyo.

Kata za Nzuguni na Ipagala wapiga kura walionekana kwa wingi wa namba tofauti na hali ilivyokuwa kwa vituo vya Kata ya Makole ambayo hata hivyo vituo vyake vilitajwa kulundikwa zaidi sehemu moja.

Baadhi ya wapiga kura wameelezwa kuridhishwa kwao na mfumo mzima wa hali ilivyo ingawa kuna changamoto ndogo ya majina kuhamishiwa vituo vingine tofauti na walivyojiandikisha lakini kila jambo linakwenda vizuri bila vikwazo.

Utulivu watawala Tabata

Hali kama hiyo ya utulivu, imetawala wakati wa shughuli ya kupiga kura karibu vituo vingi vya Tabata Kimanga, Segerea na Kinyerezi, jijini Dar es Salaam. Makundi ya watu mbalimbali, yameshuhudiwa kwenye vituo, wakipanga foleni tayari kwa kwenda kutimiza haki yao ya kupiga kura.

Maofisa mbalimbali vituoni, wameonekana wakiwasaidia wapiga kura wanaopata shida kuona majina yao, kwenye orodha ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Wapiga kura wakiwa kwenye foleni kituo Cha Tababa Kisukuru A8

Watu wenye ulemavu, nao wameonekana wakifika vituo baadhi kwa kupiga kura, ambapo wamekuwa wakipewa ruhusa ya kutangulia licha ya kukuta foleni ya watu wengine.

Changamoto pekee ambayo ilionekana kwenye baadhi ya vituo ni kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura, vikifika vituoni kuanzia saa 1:27 mpaka saa 1:30 asubuhi.

Msimamizi wa kituo cha Shule ya Kisukuru A8 Shimiyu Nkalalilwa, amesema kuchelewa kwa vifaa hivyo kulitokana na masuala ya usafiri na kufika kwenye maeneo ambayo yametengwa.

“Nikweli tulichelewa kuanza ni kutokana na mambo ya usafiri, lakini kama ulivyoona ni kama dakika 20 tu ila Sasa kama unavyoona watu wanaendelea kupiga kura,”amesema Nkalalilwa.

Hali ilivyo Vingunguti

Wakazi wa kata za Vingunguti na Segerea, Wilaya ya Ilala, Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam wameonyesha mwamko wa kushiriki uchaguzi mkuu, licha ya changamoto za baadhi ya wananchi kuchanganya vituo vya kupigia kura na kutoona majina yao katika orodha za karatasi.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi mkuu  mwaka 2025 Mtaa wa Machimbo, Kata ya Segerea, Wilaya ya Ilala, jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam akimsaidia mkazi wa eneo hilo kutafuta jina lake baada ya kufika katika kituo hicho saa 2:15 asubuhi kwa ajili ya kupiga ya kujagua Rais, mbunge na diwani.

Katika kituo cha Mtakuja, kilichopo Vingunguti, wananchi walijitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:30 asubuhi huku wakiendelea kuhamasishana kwa simu na kupitiana kwenye nyumba, wakisisitiza umuhimu wa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Akizungumza na Mwananchi, Halima Mussa amesema wamekuwa wakihamasishana kwenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua diwani wanayemtaka huku wakienda na wazee wao kwa ajili ya kuwasaidia.

“Nyumbani kwetu tumebebana wote bibi na babu yangu pamoja na wadogo zangu kuhakikisha kuwa tunapiga kura ili kumpata kiongozi wetu tena mgombea udiwani tunayemtaka,” amesema Halima.

Hata hivyo, hali ya kuchanganya vituo vya Mtakuja wamejikuta kwenye wakati mgumu kwani wamekuwa wakihangaika kutafuta majina yao kwenye orodha zilizobandikwa.

“Nimefika Mtakuja B hapa Vingunguti jina langu halipo, nikaelekezwa niende A kilichopo Titanic eneo la Reli naona mbali maana nimekuja hapa mapema baada ya kukosa jina langu na kuuliza wahusika wamenielekeza kituo kingine,” amesema Hamis Ally.

Lingine lililojitokeza ni wazee kufika katika maeneo ya vituo kuhangaika katika utafutaji wa majina hadi pale wanapoomba msaada wa kutafutiwa na wasimamizi wa uchaguzi.

Kwa upande wa kituo cha Mtaa wa Machimbo, Kata ya Segerea changamoto iliyojitokeza ni kutoyaona majina yao kwa haraka huku wengine kutoyaona kabisa licha ya kupata msaada wa kutafuta na watu wengine.

Silvia Ngowi, mkazi wa Mtaa wa Machimbo amesema amefika katika kituo hicho tangu saa 1:30 asubuhi akitafuta jina lake lakini hadi inafika saa 2:00 hajaliona hivyo kuamua kurudi nyumbani.

“Nimefika mapema ili kuepuka foleni ya baadaye lakini sijaona jina langu nimeamua nirudi nyumbani maana nimetafuta muda mrefu hadi kusaidiwa na msaidizi lakini sijaona jina langu,” amesema Silvia.

Naye, Ibrahim Daud amesema ametumia muda mrefu kutafuta jina lake hadi kupata msaada kutoka kwa msimamizi wa eneo hilo.

“Kulipata jina langu ni kipengele ambacho sikukitarajia hadi nimeomba msaada kwa wne zangu waliokuwepo hapa pamoja na kijana hapa, sasa anaenda kupiga kura kwa ajili ya kutimiza haki yangu,” amesema Daudi.

Mbali na hilo, wapo waliojitokeza kwenye vituo ambao wamejiandikishia mkoani huku wengine wakifika bila kuwa na kadi za mpiga kura na kupewa maelekezo.

“Ninakitambulisho hiki lakini sijajiandikishia hapa ilikuwa ni mkoani Arusha nataka kufahamu utaratibu ukoje kama naweza kuendelea au niondoke?,” ameuliza Ismail Mbaruku.

Hali ilivyo Moshi

Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro vituo vyote vya kupigia kura katika Jimbo la Moshi Mjini, vimefunguliwa huku Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akiwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba kupiga kura.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro wananchi 1,153,531, wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 3,074, huku hali ya usalama ikiwa imeimarishwa.

Baadhi ya wananchi wakiangalia majina yao katika kituo cha kupigia kura Kilimani, Kata ya Bomambuzi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Babu amepiga kura katika kituo cha ofisi ya kata ya Kilimanjaro ambapo amesema hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari, hivyo wananchi wajitojeze kupiga kura bila hofu.

“Leo Oktoba 29, 2025 ni siku muhimu kwetu watanzania kujitokeza kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani. Mimi tayari nimepiga kura nimetimiza haki yangu ya kikatiba, niwasihi wananchi wajitokeze kupiga kura hali ya usalama imeimarishwa,” amesema.

“Naona pia hapa kituo cha Kilimanjaro watu wamejitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba. Tunawahakikishia hali ya usalama na utulivu katika maeneo yetu,” amesema.

Akizungumza Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Moshi Mjini, Sifael Kulanga amesema mpaka sasa vituo vyote vimefunguliwa na wananchi wamejitokeza kupiga kura kutimuza haki.

Akizungumzia changamoto ya mawakala, Kulanga amesema tayari wameitatua na wote wako vituoni wakiendelea na kazi.

“Mpaka sasa hatujapata changamoto yoyote kubwa, zipo changamoto za kawaida ambazo zipo kwenye uwezo wetu kuzishughulikia. Kulikuwa na changamoto ya mawakala tumeishughulikia na mawakala wote sasa wako vituoni wanasimamia shughuli na inaenda vizuri. Niwaombe wananchi wajitokeze mapema vituoni,” amesema.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wamesema usalama umeimarishwa na mpaka sasa hakuna shida yoyote.

Grace Marealle amesema:”Zoezi limekwenda vizuri sana sisi wazee tumepewa kipaombele, wanatuangalia zaidi, hatuogopi na usalama uko vizuri kabisa wala hakuna vitisho”.

Imeandikwa na Habeli Chidawali (Dodoma), Khatibu Naheka, Devotha Kihwelo (Dar) na Florah Temba (Moshi)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *