Mashambulizi yaliyofanywa leo na Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza yameua Wapalestina wasiopungua 100, wakiwemo watoto 35, ukiwa ni ukiukaji wa hivi karibuni wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na utawala huo ghasibu.

Mauaji ya idadi hiyo ya watu yameripotiwa katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumatano na msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Gaza, Mahmoud Basal, huku ndege za kivita za Israel zikiendelea kufanya mashambulizi makali ya anga katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Rafah katika sehemu za kusini mwa eneo hilo la Palestina linalozingirwa.

“Katika kipindi cha chini ya saa kumi na mbili, vikosi vya jeshi la utawala uvamizi wa Israel vimefanya mauaji ya kutisha dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza, na kuua zaidi ya watu 100, wakiwemo watoto 35, na kurekodi uhalifu mwingine dhidi ya watu wetu,” amesema afisa huyo.

Mashambulizi ya anga ya Israel yamelenga Jiji la Gaza, Khan Yunis na kambi za wakimbizi za katikati mwa eneo hilo, yakishambulia nyumba, mahema ya wakimbizi, na hospitali.

Madaktari wameonya kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka, huku raia wengi wakiwa wamejeruhiwa vibaya na wengine wamekwama chini ya vifusi.

Baada ya karibu saa 12 za mashambulizi makali ya mabomu, Israel ilidai kuwa imerejesha usitishaji mapigano saa 4 asubuhi kwa wakati wa Gaza.

“Mauaji haya yanafanywa mbele ya macho ya wapatanishi na jamii ya kimataifa, ambayo inaendelea kubakia kimya na haiwezi kuchukua hatua yoyote ya maana ya kukomesha umwagaji damu ambao unaendelea kwa zaidi ya miaka miwili,” Basal aliongeza.

Wapalestina wasiopungua 100 wameuawa leo Ukanda wa Gaza

Israel, ambayo imekuwa ikishambulia Ukanda wa Gaza mara kwa mara kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano, iliilaumu Hamas kuwa imekiuka makubaliano hayo, ikidai kundi hilo lilishambulia wanajeshi wa utawala huko huko Rafah siku ya Jumanne, na kwamba mwanajeshi mmoja aliuawa.

Hamas imekadhibisha shutuma hizo, ikiilaumu Tel Aviv kuwa imenaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Gaza, Mahmoud Basal amesema: “Kinachotokea Gaza leo ni aibu kwa ubinadamu na kinaonyesha kwamba jamii ya kimataifa, kupitia ukimya wake, inashiriki katika uhalifu huu.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *