Shughuli za upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa Tanaznia zimeendelea vizuri na kwa amani kwa kikasi kikubwa licha ya ghasia na machafuko madogo yanayoripotiwa huku na kule.

Watanzania waliotimiza masharti ya kupiga kura leo walielekea katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais, Wabunge na madiwani katika uchaguzi uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA na kushirikisha vyama vingiine vingi vya siasa.

Rais Samia Suluhu Hassan anatazamiwa kushinda muhula wa pili hasa baada ya chama kikuu cha upinzani kususia uchaguzi huo. 

Baadhi ya ripoti zinasema Polisi wamekabiliana na ‘waandamanaji’ jijini Dar es Salaam wakati kura zikiendelea kupigwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Polisi jijini Dar es Salaam wametawanya kundi la vijana waliokuwa wakijaribu kuandamana katika maeneo ya Ubongo na Kimara eneo la Kibo.

Mapema leo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Chalamila, amesema vyombo vya dola viko imara na tayari kukabiliana na jaribio lolote la uvunjifu wa amani katika jiji hilo, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga utulivu.

Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania ametangaza amri ya kutotoka nje jijini Dar es Salaam kuanzia leo saa kumi na mbili jioni.

Wapiga kura Uchaguzi Mkuu Tanzania

”Jeshi la polisi linawatangazia wakaazi wote wa jiji la Dar es Salaam kuwa kuanzia leo tarehe 29 Oktoba mwaka 2025 kuanzia saa kumi na mbili jioni wawe majumbani mwao,” alisema Camillus akitoa tangazo hilo.

Hayo ni kufuatia matukio ya ghasia yaliyoshuhudiwa katika maeneo kadhaa mjini Dar es Salam na kwingineko nchini humo ambapo waandamanaji wanaopinga kufanyika kwa uchaguzi wameandamana wakifunga barabara na kuchoma moto maeneo kadhaa.

Waandamanaji waliwasha moto barabarani, kuharibu mabasi, na kusababisha uharibifu kwenye vituo vya mabasi ya mwendo kasi na miundombinu mingine ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *