Jeshi letu la Polisi ni miongoni mwa vyombo muhimu vya kiutendaji vinavyohusika moja kwa moja na ulinzi wa Rais pamoja na usalama wa mali zake.

Kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu, chombo hiki kinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa haki na weledi wa hali ya juu.

Ni matarajio ya Watanzania wote kwamba Jeshi la Polisi litafanya kazi kwa umahiri na uadilifu wa hali ya juu.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa Jeshi hili linaongozwa na wanadamu, na wanadamu kama tunavyoelewa sote, hakuna aliyekamilika, ukamilifu ni sifa ya Mwenyezi Mungu pekee. Kwa msingi huo, ni jambo la kawaida kuona changamoto au makosa ya kibinadamu yakijitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Polisi.

Kuna nyakati Jeshi letu linajikuta limeshindwa kutatua baadhi ya matukio ya kihalifu, jambo ambalo si la kushangaza kwa kuwa halijaongozwa na malaika, bali binadamu.

Katika mazingira hayo, haitakuwa busara kwa Jeshi letu kushupaza shingo na kukataa udhaifu wake. Badala yake, linapaswa kukubali kuwa kuna maeneo linayoshindwa na hivyo likubali kupokea msaada kutoka kwa wadau wengine wenye uwezo.

Naamini kabisa kuwa wapo Watanzania wengi walio nje ya mfumo rasmi wa Jeshi la Polisi lakini wana uwezo mkubwa wa kusaidia katika masuala ya kiuchunguzi.

Miongoni mwao ni waandishi wa habari za uchunguzi pamoja na vyombo vya habari kwa ujumla, mhimili wa nne usio rasmi katika utawala wa kidemokrasia.

Moja ya maeneo ambayo Jeshi letu la Polisi limeonekana kuwa dhaifu ni katika kukabiliana na watu au vikundi vinavyojulikana kama wasiojulikana.

Hawa wamehusishwa na vitendo vya kihalifu vya kuteka, kutesa, kuua au kupoteza watu katika mazingira ya kutatanisha.

Matukio haya yamekuwa yakijirudia mara kwa mara, huku wahusika wakibaki kuwa ‘wasiojulikana.’

Vitendo hivi havikuanza leo. Tokea enzi za Rais Jakaya Kikwete, tulishuhudia tukio la kutekwa kwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha madaktari, Dk Steven Ulimboka, ambaye alifanyiwa ukatili wa kutisha.

Kadhalika, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absolom Kibanda, naye alitekwa na kujeruhiwa vibaya, lakini hadi leo wahusika hawakuwahi kufahamika.

Katika awamu ya tano, hali ilizidi kuwa mbaya. Mwandishi wa habari za uchunguzi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na hajawahi kupatikana hadi leo.

Mwanaharakati Ben Saanane naye alitoweka pasipo maelezo. Mbunge na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alipigwa risasi mchana kweupe katika eneo la makazi salama ya wabunge yakiwa na ulinzi wa saa 24 na kamera za CCTV.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilishindwa kuchukua hatua madhubuti au kutoa majibu ya kuridhisha.

Hata hivyo, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, vitendo hivi vilianza kupungua, na hali ya utulivu ilianza kurejea. Lakini wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, dalili za kurejea kwa vitendo hivi zimeanza kujitokeza tena.

Hili linaibua maswali mazito; Je, Jeshi la Polisi lina uwezo wa kweli wa kuwabaini hawa wasiojulikana? Au tumefika mahali kundi hili linajivinjari waziwazi bila hofu yoyote?

Leo hii, kuna taarifa za watu wanaojitambulisha kuwa polisi kusimamisha magari, kuwashusha abiria na baadaye miili yao kupatikana ikiwa imeuawa kwa ukatili mkubwa.

Mfano hai ni wa Mzee Salim Kibao wa Chadema, aliyeshushwa kwenye gari na baadaye mwili wake kuokotwa ukiwa umefanyiwa ukatili wa kutisha.

Rais mwenyewe alilazimika kuagiza uchunguzi wa haraka, lakini hadi leo hakuna majibu.

Wapo pia waliopigiwa simu na kuitwa polisi, kama ilivyomtokea Soka wa Chadema ambaye baada ya kuitika wito, hakuwahi kurejea nyumbani.

Mdude Nyangali naye alichukuliwa mbele ya familia yake na watu waliodai ni polisi, akapigwa, akatekwa na kupotea kwa muda mrefu.

Matukio haya sasa yamefika hata kwenye hoteli za kifahari zenye CCTV kila kona. Wageni wanatekwa, wanawake kubakwa, wanaume kulawitiwa na baadaye kutupwa mipakani mwa nchi zao.

Ni wazi kuwa Jeshi letu la Polisi haliwezi kila kitu, kama ambavyo hakuna taasisi inayoweza kufanya kila jambo kikamilifu peke yake.

Ikiwa tumeshindwa kuendesha baadhi ya maeneo kama bandari na tukakubali msaada kutoka DP World, ikiwa tunaendelea kushirikiana na mataifa mengine kuendeleza ATC na SGR, basi pia hatupaswi kuona aibu kuomba msaada kwenye masuala ya kiuchunguzi.

Kama Jeshi letu la Polisi linashindwa kuwatambua wasiojulikana, linaweza kutangaza wazi hali hiyo na kuomba msaada kutoka taasisi za kimataifa kama Scotland Yard, au hata kushirikiana na wachunguzi binafsi. Tusikubali hali ya nchi yetu ambayo ni kisiwa cha amani kuchafuka kwa sababu ya kundi dogo lisilojulikana ambalo linavuruga taswira ya taifa letu mbele ya macho ya dunia. Kwa pamoja tuseme hapana, inatosha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *