Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na 30 Oktoba 2025.
Miaka 134 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran.
Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na Hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu Hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza chuo kikuu cha kidini cha Isfahan.
Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat na Hashiyatu Sharhil Lum’ah.

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri.
Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu.
Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henry Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.
Dunant alizaliwa Geneva, Uswisi na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita.
Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Aban 1359 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.
Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia.
Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa.
