Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulizi makubwa ya anga ya utawala wa Israel katika maeneo mbalimbali ya kusini, katikati na kaskazini mwa Gaza.

Ismail Baghaei ameashiria historia ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya ukiukaji mkubwa wa kanuni na misingi yote ya kisheria na kimaadili na kusema: Mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel katika kipindi cha saa 24 zilizopita dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ghaza yanayofanyika kwa amri ya moja kwa moja ya Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu yanakinzana wazi na makubaliano ya usitishaji vita, ni ishara nyingine ya azma mahususi ya Tel Aviv ya kuendelea na operesheni zake za mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na hali hii inaongeza maradufu wajibu wa serikali zote, kwa mujibu wa “Mkataba wa Kuzuia adhabu na mauaji ya Kimbari”, kwa ajili ya kukomesha jinai za utawala huo na kuwaadhibu wahalifu.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria kuendelea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa kuzingatia uungaji mkono mpana wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na akasisitiza wajibu maalumu wa wadhamini wa usitishaji vita wa kukomesha uanzishaji vita na mauaji ya kimbari ya utawala huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *