
Rais Donald Trump wa Marekani ameiagiza Wizara ya Vita ya nchi hiyo kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia; katika uamuzi ambao umewatia wasiwasi wapinzani wa silaha za maangamizi ya umati na wataalamu masuala ya usalama duniani.
Mapema leo Alhamisi Trump ametuma ujumbe katika jukwaa lake la kijamii la Truth Social akisema kuwa ametoa agizo hilo kwa kufuatia majaribio ya silaha hizo yanayofanywa na nchi nyingine. Amesema mchakato huo utaanza mara moja.
Rais wa Marekani amezitaja Russia na Uchina kama nchi mbili zenye nguvu kubwa zaidi za nyuklia duniani, akidai kwamba ikiwa Washington haitaaanza kufanya majaribio ya silaha za nyuklia nchi hizo zitafanikiwa “ndani ya miaka mitano.”
Mchakato wa Marekani wa kuzifanyia majaribio silaha za nyuklia unatarajiwa kutoa data kuhusu utendaji wa vichwa vipya vya nyuklia na iwapo hifadhi kongwe za silaha hizo zinaweza kutegemewa.
Matamshi haya ya Trump yanaashiria wito wa moja kwa moja wa Marekani wa kufanywa majaribio mapya ya nyuklia tangu Washington ilipofanya jaribio lake la mwisho mwaka 1992.
Wakosoaji kwa upande wao wametahadharisha kuwa kuhuisha majaribio ya moja kwa moja ya silaha za nyuklia kutavuruga jitihada za miongo kadhaa kuzuia usambazaji wa silaha hizo na kuruhusu majaribio mtawalia ya kulipiza kisasi kote ulimwenguni, na hivyo kuathiri Mkataba Unaopiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBT).
Marekani ilifungua zama za nyuklia mwezi Julai mwaka 1945 kwa kudondosha bomu la nyuklia la kilotani 20 huko Alamogordo, Mexico, na wiki kadhaa baadaye ikahambulia miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan kwa silaha za nyuklia.