Ripoti hiyo SOFA 2025 inatoa ujumbe ulio wazi uharibifu wa ardhi si suala la mazingira pekee unaathiri uzalishaji wa kilimo, maisha ya vijijini, na usalama wa chakula.

SOFA 2025 inatoa uchambuzi wa kina zaidi hadi sasa kuhusu jinsi uharibifu wa ardhi unaosababishwa na binadamu unavyoathiri mavuno ya mazao, inatambua maeneo yaliyo hatarini zaidi duniani, na kuchunguza jinsi hasara hizi zinavyohusiana na umaskini, njaa na utapiamlo.

Kwa kutumia takwimu za hivi karibuni kuhusu usambazaji wa mashamba, ukubwa wake, na uzalishaji wa mazao, ripoti hiyo inaonesha fursa zinazoweza kuchukuliwa kupitia mbinu endelevu za matumizi ya ardhi na usimamizi wake, pamoja na sera maalum za kusaidia hatua hizo. Hatua hizi zinalenga kuepuka, kupunguza, na kurejesha ardhi iliyoharibiwa huku zikiboresha uzalishaji wa chakula na maisha ya wakulima.

“Ili kunufaika na fursa hizi, lazima tuchukue hatua kwa uthabiti. Usimamizi endelevu wa ardhi unahitaji mazingira wezeshi yanayohamasisha uwekezaji wa muda mrefu, ubunifu, na uwajibikaji,” ameandika Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, katika dibaji ya ripoti hiyo.

Athari za uharibifu wa ardhi

FAO imefafanua uharibifu wa ardhi kama kupungua kwa muda mrefu kwa uwezo wa ardhi kutoa huduma muhimu za ikolojia na mazingira.

Uharibifu wa ardhi husababishwa na mchanganyiko wa vichocheo vya asili (kama mmomonyoko na chumvi kupita kiasi) na shinikizo la shughuli za binadamu kama ukataji miti, ufugaji kupita kiasi, na kilimo kisicho endelevu.

Ripoti ya SOFA 2025 inatumia mbinu ya “deni la uharibifu” kupima kiwango cha uharibifu kwa kulinganisha viashiria vitatu kaboni ya kikaboni, mmomonyoko, na maji kwenye udongo na hali ya asili bila ushawishi wa binadamu, kwa kutumia mfumo wa kujifunza kwa mashine.

Matokeo yanaonesha kuwa watu bilioni 1.7 wanaishi katika maeneo yenye upungufu wa mavuno kwa 10%, na watoto milioni 47 wanakabiliwa na udumavu. Asia imeathirika zaidi kutokana na wingi wa watu na kiwango kikubwa cha uharibifu.

Hata hivyo, kurejesha asilimia 10 ya ardhi iliyoharibiwa kunaweza kuongeza uzalishaji wa chakula wa kutosha kulisha watu milioni 154 zaidi kila mwaka.

Ripoti imetoa wito wa sera jumuishi za matumizi ya ardhi zikiwemo udhibiti wa ukataji miti, motisha za kiuchumi, na ruzuku zinazohusishwa na matokeo ya kimazingira. Inasisitiza pia umuhimu wa sera zinazozingatia tofauti kati ya wakulima wadogo na wakubwa ili kukuza kilimo endelevu na kupunguza uharibifu wa ardhi.

Jukumu la FAO

Jumuiya ya kimataifa imetambua uharibifu wa ardhi kama changamoto kuu ya dunia, ambapo zaidi ya nchi 130  zimeahidi kufikia “Utoaji wa Ardhi Usio na Uharibifu” (Land Degradation Neutrality) chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na Jangwa (UNCCD).

FAO iko mstari wa mbele katika juhudi za kuzuia, kupunguza na kurejesha uharibifu wa ardhi kupitia ukusanyaji wa data, mwongozo wa sera, na miradi ya utekelezaji mashinani.

Kama taasisi inayosimamia kiashiria cha SDG namba 2 (Kukomesha Njaa), FAO hufuatilia na kusasisha usambazaji wa kimataifa wa tofauti za mavuno kwa kutumia mfumo wake wa Global Agro-Ecological Zoning (GAEZ v5) ambao umetumika katika ripoti hii. Pia hutoa taarifa muhimu kuhusu afya ya udongo kupitia Ramani ya Kimataifa ya Kaboni ya Kikaboni ya Udongo (GSOC Map).

“Mnamo mwaka 2025, FAO inathibitisha upya dhamira yake ya kusimamia ardhi kwa njia endelevu. Toleo hili la Hali ya Chakula na Kilimo ni sehemu ya dhamira hiyo  kutoa msingi kamili wa ushahidi ili kuongoza sera, uwekezaji, na hatua katika ngazi zote,” ameandika Mkurugenzi Mkuu wa FAO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *