Taarifa hiyo kutoka tawi la kijeshi la Hamas imetolewa saa kadhaa baada ya Israel kuikabidhi miili 45 ya Wapalestina. Kubadilishana miili ya mateka na Wafungwa kati ya Israel na Hamas kunaashiria hatua nyingine chini ya makubaliano yaliyoratibiwa na Marekani kwa lengo la kuumaliza mzozo mbaya zaidi kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.
Tangu usitishaji vita ulipoanza kutekelezwa wanamgambo wa Hamas wameshakabidhi miili ya mateka 20 kwa Palestina wakati miili ya mateka wengine 8 ikiwa bado iko Gaza.
Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa leo Jumanne umetoa taarifa kwamba umeshasambaza vifurushi vya chakula kwa watu milioni 1 kwenye Ukanda wa Gaza tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipoanza kutekelezwa tarehe 10 mwezi uliopita. Hata hivyo umoja huo umeonya kuwa bado unapambana kuokoa maisha ya watu.
Shirika la WFP lataka njia zaidi zifunguliwe ili kufikisha misaada Gaza
Zaidi Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP kupitia Mkurugenzi wake kwa Palestina Antoine Renard, limesisitiza kuwa vivuko vyote vinavyoingia Ukanda wa Gaza vinapaswa kufunguliwa ili kuingiza misaada kwenye eneo hilo linalokabiliwa na njaa.
Renard amesema kuwa, “Shirika la Mpango wa Chakula linaweza kuhakikisha kuwa watu wanapata chakula wanachokihitaji na tayari tumewafikia watu milioni moja. Lakini hiyo haitoshi. Tunahitaji vivuko vingi zaidi vifunguliwe na kuwe na uwezekano bora zaidi wa kuifikia Gaza. WFP inahitaji kutumia barabara zote muhimu ili kuleta chakula. “
Shirika hilo la chakula linalenga kuwafikia wakaazi milioni 1.6 wa Ukanda wa Gaza kwa vifurushi vya chakula ambavyo vinatosha kulisha kila familia kwa kipindi cha siku kumi. Inakadiriwa kuwa takriban wakaazi 700,000 wa Gaza sasa wanapata mikate kila siku iliyookwa katika maduka yanayosaidiwa na Shirika hilo la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa.
Juhudi za kuilisha Gaza zinaendelea wakati timu zilizo chini ya Idara ya ulinzi wa raia katika maeneo mengi ya ukanda huo wanaendelea kufanya kazi ya kuondoa vifusi na hatari zinazotokana na nyumba zilizoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel.