Bi. Tipo ambaye pia ni Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania amesema hayo wakati wa mahojiano mahsusi kuhusu miaka 80 ya shirika hilo sambamba na siku ya chakula duniani, Oktoba 16, maadhimisho ambayo kwa Kenya yalifanyika Oktoba 28.

Anasema kwamba, “wakulima wawe macho watumie teknolojia mpya na waendane na uhalisia wa kilimo cha sasa. Hii ni fursa ya kufanya vitu kwa njia tofauti.”

Ametoa kauli hiyo wakati huu ambapo FAO Kenya imekuwa mstari wa mbele kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo kupitia miradi mbali mbali ili hatimaye kuongeza uzalishaji wa chakula ambao hautegemei juhudi za wakulima pekee bali pia usimamizi wa ardhi.

Nafaka mbalimbali zinazozalishwa kupitia kilimo-ikolojia.

@FAO/Joseph Othieno

Nafaka mbalimbali zinazozalishwa kupitia kilimo-ikolojia.

Mfumo wa GIS na usimamizi wa ardhi

Ndiyo maana FAO Kenya imejitosa kusaidia serikali ya Kenya kuboresha matumizi ya teknolojia ya Geographic Information System (GIS) ili kuongeza ufanisi wa upangaji na uendelezaji wa ardhi ambapo Bi. Tipo amesema utekelezaji wa teknolojia hii umeleta manufaa makubwa kwa sekta ya kilimo.

“Ukichunguza kazi ya urejeshaji wa ardhi na usimamizi wa ardhi, tumeweza kufanya mambo mengi sana. Tuna wahitimu wa GIS ambao sasa wamepata mafunzo ya kusimamia maabara za GIS tulizozipatia kaunti 47 za nchi hii. Kupitia mafunzo haya, wataweza kuchora ramani na kufanya upangaji wa ardhi katika kila kaunti,” amesema.

Ameongeza kuwa mpango huo unasaidia sio tu kupanga matumizi bora ya ardhi, bali pia unaimarisha usimamizi wa rasilimali ardhi za kilimo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mfumo wa KIAMIS waongeza uwazi na usajili wa wakulima

Maafisa wa FAO wakimbelea mkulima aliyejisajili chini ya mradi wa KIAMIS huko kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya.

@FAO/Joseph Othieno

Maafisa wa FAO wakimbelea mkulima aliyejisajili chini ya mradi wa KIAMIS huko kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya.

Mbali na teknolojia ya GIS, Bi. Tipo alitaja Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Taarifa za Kilimo nchini Kenya (KIAMIS) kama hatua nyingine muhimu iliyowezeshwa na FAO kwa kushirikiana na serikali.

“Mpango huu umeweza kusajili zaidi ya wakulima milioni 6.5. Kupitia usajili huu, serikali inapata urahisi wa kujua ni nani anayefanya shughuli gani za kilimo na jinsi wanavyoweza kunufaika na ruzuku na huduma nyinginezo,” amefafanua.

Kwa mujibu wake, mifumo hii miwili—GIS na KIAMIS—imeleta mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku serikali ya Kenya ikijivunia mafanikio hayo ya kidijitali.

Ujumuishaji wanawake na vijana

Licha ya mafanikio haya, Bi. Tipo amesisitiza kuwa bado kuna pengo kubwa katika upatikanaji wa huduma na fedha hasa kwa wanawake.

“Tunapaswa kuwajumuisha wanawake wengi zaidi kwenye sekta ya kilimo na kuwapa teknolojia rafiki kwa wanawake. Vivyo hivyo, tunapaswa kuwavutia vijana kupitia teknolojia wanazozikubali,” amesema.

Akitofautisha zama za sasa na za zamani, amesema vijana hawawezi tena kuhamasishwa kwa kutumia zana za kizamani kama jembe, bali wanahitaji mbinu za kisasa kama matumizi ya droni, akili mnemba, na uvumbuzi mwingine wa kidigitali.

Mwakilishi wa FAO nchini Kenya, Nyabenyi Tito Tipo akizungumza na wadau na wakulima wakati wa maadhimisho ya siku ya chakula duniani huko kaunti ya Homa Bay Oktoba 28, 2025.

Mwakilishi wa FAO nchini Kenya, Nyabenyi Tito Tipo akizungumza na wadau na wakulima wakati wa maadhimisho ya siku ya chakula duniani huko kaunti ya Homa Bay Oktoba 28, 2025.

Kilimo si kukwatua jembe peke yake

Kwa vijana, amewataka kuchangamkia fursa zilizomo katika minyororo ya thamani ya kilimo badala ya kuangalia tu upande wa uzalishaji shambani.

“Kilimo si kukwatua ardhi peke yake. Unaweza kuwa msafirishaji, au kutumia simu ya kiganjani kuunganisha watu katika biashara ya mazao,” ameongeza.

Kwa wawekezaji, amewahimiza kutazama kilimo kama sekta yenye fursa kubwa za kibiashara, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa karibu na wakulima.

“Ni vema wawekezaji waboreshe mazingira ya ushirikiano ili kila upande unufaike,” ametamatisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *