Dar es Salaam. Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Ambwene Yessayah ‘AY’ ameweka wazi imani yake kwenye muziki kwa sasa akidai unahitaji uwekezaji zaidi.
AY amesema uwekezaji umekuwa kitu cha kwanza kuliko sanaa yenyewe.
“Uwekezaji umekuwa kitu cha kwanza kuliko hata sanaa yenyewe. Kuna wasanii wengi wazuri wana sanaa nzuri lakini wanakosa uwekezaji. Uzuri kuna wadau siku hizi naona wanajaribu kuangalia vipaji vya vijana hapa waendelee kuwapa nafasi zaidi,” amesema AY.
Amesema wasanii wamebahatika kuwa na vitu vingi vinavyoweza kuwasadia. Inabidi wajitahidi kufanya kazi kwa ukubwa ikiwemo kuandaa video na kolabo kali.
” Mfano kwenye kolabo ni kuzifanya ziwe na watu wenye ujuzi zaidi. Inabidi tutengeneze video kali zaidi, kwenye audio. Pia watu wengine huwa wanapiga mixing basi, lakini kuna mastering pia ili ukipeleka kwenye vyombo vya nje unaweza kuwa na wimbo mzuri lakini hauna ubora.
“Naona kila kitu kinaenda poa tangu zamani nilikuwa nahutubia sana kwenye uwekezaji ambao sasahivi naona unafanyiwa kazi. Lakini kama tungeanza kufanya tangia zamani muziki ungeamka zaidi ya hapa,” amesema AY.
Amesema kuna rekodi nyingi aliweka kwenye muziki wa Bongo lakini hazikuhifadhiwa vizuri kwaajili ya vizazi vya sasa.
“Hiyo pia ni shida nyingine watu kutoweka rekodi. Unakuta mtu unatengeneza kitabu kiweze kuweka rekodi vizuri hata media taarifa nyingi zinatolewaga naangalia nasema hata hii jamani,” amesema AY.
Ameweka wazi kolabo zake alizofanya miaka ya 2010 na filamu aliyoigiza na mastaa wakubwa duniani.
“Mimi meneja wangu ni Mmarekani tangu 2003 mpaka leo na hata kwenye movie kanipeleka yeye. Imetoka inaitwa Demon Pitt ipo Amazon, imetoka mwaka 2025.
“Yupo Richard Glecko, yupo Superman, yupo jamaa wa Expendable, nilipata uzoefu mkubwa wakati wa kushuti,” amesema AY.