Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Sheilah Jepngetich amezungumza na Salome Gatakaa Araka ambaye ni Mwakilishi wa FODDAJ na akamueleza walianzia wapi harakati zao.
“FODAJ ilianza na uundaji wa ufahamu yaani sera na uchechemuzi kumaanisha kwamba kuwe kutengwa kwa fedha za kutengeneza mahali pa waathiriwa kuishi, na pia kusisitiza ufahamu wa kutetea wale ambao wametengwa. Katika kata ya Kajiado, tumesukuma sera za GBV ili kuimarisha juhudi za kuzuia waathiriwa kuumia zaidi.”
Pamoja na kukabili ukatili wa kijinsia, Salome akaeleza namna wanavyo wajengea wanawake uwezo wa kujitegemea. “FODDAJ imekuwa mstari wa mbele katika katika kupaza sauti za wanawake na wasichana, na pia kuhimiza akina mama kuweka akiba za vikundi, kushirikiana na kusaidiana ili kujikimu kiuchumi. Tumehimiza akina mama kuweka akiba kwa vikundi vya maendeleo, kushirirki mafunzo ya ujasiriamali na kushirikiana na wengine kwa pamoja. Na pia wanafundishwa mambo tofauti kama vile kutengeneza nywele , kusoma na kuandika na pia na kuhesabu.”
Mmoja wa wanufaika wa FODDAJ ni Geraldine Ndayisenga mkazi wa Kitengela ambaye ni manusura wa ukatili na anasema “Mimi ni mmoja wa wale waliopitia dhuluma. Nilijua kuhusu FODDAJ kupitia rafiki yangu. Nikasaidiwa, nilipata matibabu, nikapata ushauri kwa mwezi mmoja. Baada ya hapo nikajiunga na mafunzo ya kutengeneza nywele, makucha na ushonaji. Mafunzo hayo yamenisaidia sana, sasa najisikia niko huru na nina furaha kuwa sehemu ya jamii tena. Fodaj Foundation imenishika mkono na kunionesha namna bora ya kuishi hapa Kitengela. Wamenisaidia kwa mambo mengi, na kwa kweli maisha yangu yamebadilika kwa njia chanya sana.”
Ushirikiano na Serikali
Bi. Araka, anaeleza namna wana ushirikiano na serikali na mashirika ya kiraia. “Kwa kushirikiana na serikali na mashirika mengine ya kiraia, waathirika wanapatiwa msaada kwa ajili ya huduma za afya. Mfano wale waliobakwa au kupigwa, hupata matibabu kwa vipimo au dawa. Aidha, waathirika wa kimawazo wanapewa msaada wa kisaikolojia ili iwasaidie kuondokana na madhara ya kiwewe baada ya dhuluma ambayo wamepitia.