CHADEMA imeandika katika mtandao wake wa X kwamba, Makamu mwenyekiti wa chama hicho John Heche, aliyekamatwa Oktoba 22 amefunguliwa mashtaka ya makosa ya ugaidi. Chama hicho kimesema polisi ilimsafirisha Heche kutoka mji mkuu Dodoma hadi Kinondoni, alikofunguliwa mashtaka hayo.
Kwa mujibu wa CHADEMA, Heche alikataa kuandika taarifa lakini ikasema atatekeleza haki yake hiyo wakati atakapopelekwa kortini. Hadi sasa haijawa wazi ni lini hasa Heche atakapofikishwa mahakamani.
Awali makundi ya kutetea haki za binaadamu yalielezea wasiwasi wao kuhusu kamata kamata, iliyokuwa ikifanyika dhidi ya upinzani kuelekea Uchaguzi wa Oktoba 29. Viongozi wa upinzani aidha walifungiwa jela au kunyimwa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo mkuu.
Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Antiphas Mughwai Lissu, hadi leo (05.11.2025 ), anazuiliwa jela akikabiliwa na mashtaka ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania INEC, Rais Samia Suluhu Haassan alishinda Uchaguzi wa Oktoba 29, kwa asilimia 98 ya kura, matokeo ambayo upinzani umeyapinga na kuutaja uchaguzi huo kuwa mchezo wa kuigiza.
Ghasia za baada ya uchaguzi zilijitokeza siku ya Uchaguzi, vijana walipomiminika barabarani kupinga uchaguzi huo ambao haukuvishirikisha vyama vikuu viwili vya upinzani, CHADEMA na ACT Wazalendo upande wa Tanzania Bara.
Miili ya waandamanaji yadaiwa kutupwa Mto Ruvu
Kuchacha kwa maandamano hayo, kuliifanya serikali kufungia mitandao na kuweka amri ya kutotoka nje masaa ya jioni. Upinzani unasema katika vurugu hizo, mamia ya watu waliuwawa lakini hadi sasa imekuwa vigumu kuthibitisha idadi ya waliouwawa kutokana na viongozi husika, kutopatikana kuzungumza na vyombo vya habari.
CHADEMA Kupitia afisa wake anayeshughulikia masuala ya kigeni Deogratius Munishi, pia imedai kuwa vikosi vya usalama vimekuwa vikiitupa miili ya mamia ya maelfu ya waliouwawa katika ghasia hizo, vikijaribu kuficha kiwango cha mauaji yaliyofanywa.
“Kwa siku kadhaa zilizopita tumesikia ripoti kwamba polisi wanakwenda katika hospitali mbalimbali, wakikusanya miili ya wale waliouawa wakati wa maandamano, na tunasikia baadhi inazikwa katika makaburi ya pamoja. Haya ndio mambo tunayotaka mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa kuja kujionea. Tunasikia baadhi ya miili inatupwa katika bahari hindi, mingine inatupwa katika Mto Ruvu, ambao ni maarufu kuwa una mamba wengi. Kwa hivyo unapoitupa miili hiyo inakuwa ndio chakula cha mamba,” alisema Munishi.
Serikali yaendelea na shughuli za kiutawala
Serikali ya Samia Suluhu Hassan bado imekaa kimya pia kuhusu hili. Hakuna maoni yoyote yaliyotolewa kuhusu madai hayo.
Haya yanajiri wakati kiongozi huyo wa taifa hilo la Afrika Mashariki akiwaita wabunge wote wateule mjini Dodoma Novemba 8 kuanzisha shughuli za usajili na taratibu nyengine za kiutawala, zitakazoanza rasmi kuanzia siku ya Jumamosi hadi siku ya Jumatatu Novemba 10, 2025.
