Iran imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana kwa dharura kufuatia kauli za “kushtua sana” zilizotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia.

Iran imeonya kuwa kauli hizo ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na zinakiuka wajibu wa Marekani chini ya sheria za kimataifa.

Katika barua iliyoandikwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais wa Baraza la Usalama Michael Imran Kanu, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani alikosoa kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani kuhusu majaribio ya silaha za nyuklia.

Iravani amebainisha kuwa mnamo Oktoba 29, 2025, Rais wa Marekani alitangaza hadharani kupitia mitandao ya kijamii kuwa ameagiza Wizara ya Vita “kuanza majaribio ya silaha za nyuklia sawa na mataifa mengine yenye silaha hizo,” na kutangaza kuwa “mchakato utaanza mara moja.”

Balozi huyo ameongeza kuwa katika mahojiano ya baadaye na kipindi cha 60 Minutes cha CBS mnamo Oktoba 31, 2025, Rais huyo alisema kuwa silaha za nyuklia ambazo Marekani inamiliki hivi sasa “zina uwezo wa kuharibu dunia mara 150.”

Barua hiyo ilieleza kuwa kauli hizo ni ukiukaji wa wazi wa wajibu wa Marekani chini ya Kifungu cha VI cha Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), na zinadhoofisha roho ya Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBT).

Iravani pia alilaani Marekani kwa kile alichokiita kampeni ya “uongo na upotoshaji” inayolenga kupotosha kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ambao ni wa amani.

Barua hiyo pia ilirejelea “kitendo cha uchokozi” kilichofanywa na Marekani dhidi ya Iran tarehe 24 Juni 2025. Katika uchokozi huo Marekani ilishambulia  vituo vya nyuklia vya Iran, hatua ambayo Iravani ameitaja kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Iran imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuchukua hatua kwa mujibu wa wajibu wake wa kulinda “amani na usalama wa kimataifa.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *