Hayo yanajiri wakati Marekani ikiandika rasimu ya azimio la Umoja wa Mataifa litakalotowa idhini ya kuundwa baraza la mpito la uongozi na kikosi cha wanajeshi wa kimataifa kwenye Ukanda huo. 

Mabaki ya mwanajeshi Italy Chen, aliyetiwa nguvuni na wanamgambo wa Kipalestina mnamo Oktoba 2023 yalikabidhiwa jana, Jumanne, jioni kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji wa mapigano ya Gaza yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump wa Marekani.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilisema kwenye taarifa yake na hapa nainukuu: “Kufuatia kukamilika kwa utaratibu wa utambuzi, wawakalishi wa jeshi la wameifahamisha familia ya Sajenti Italy Chen, kwamba mpendwa wao amerejeshwa Israel na ametambuliwa kuwa ni yeye.” Mwisho wa kunukuu.

Chen, Muisraeli mwenye pia uraia wa Marekani, alikuwa akilinda mpakani wakati wanamgambo wa Kipalestina walipofanya uvamizi wao wa tarehe 7 Oktoba 2023.

Alituma ujumbe wa mwisho wa wazazi wake wakati uvamizi huo ulipoanza, lakini jeshi la Israel lilitangaza kkifo chake miezi mitano baadaye, mnamo Machi 2024.

Tawi la kijeshi la Hamas, Al-Qassam Brigade, lilisema hapo jana kwamba mwili wa Chen ulipatikana kwenye kiunga cha Shujaiya mashariki mwa Jiji la Gaza wakati wa operesheni inayoendelea ya kusaka miili ya mateka.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, amesema watahakikisha kuwa wanakamilisha operesheni hiyo na kuikabidhisha miili yote ya mateka licha ya ugumu na vikwazo vilivyopo.

Kuanzishwa kwa serikali ya muda Gaza

Hayo yakijiri, Marekani imetangaza rasimu ya kwanza ya azimio la Umoja wa Mataifa linalodhamiria kuanzisha serikali ya muda ya Gaza na kikosi cha kimataifa kulinda amani kwenye Ukanda huo.

Mji wa Gaza - 2025 | Mahema ya makaazi
Mji wa Gaza baada ya wakaazi wake kurejea na kuweka mahema kama makaazi.Picha: Omar Al-Qattaa/AFP

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani amesema kwa sasa majadiliano na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wajumbe wengine muhimu wa Umoja huo yamejikita juu ya namna ya kuutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na Rais Trump.

Rasimu hiyo ya kurasa mbili inazungumzia jinsi kile kiitwacho Baraza la Amani litakavyoiongoza Gaza katika kipindi cha mpito na kuanzisha Kikosi cha Kimataifa cha Utulivu, ISF, ambacho kitakuwa na mamlaka ya kuwalinda raia, na kusimamia usambazaji wa misaada ya kibinaadmu na kulinda maeneo ya mpaka wa Gaza na Israel na Misri.

Bado haijafahamika ikiwa rasimu hiyo itaungwa mkono na mataifa mengine wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hasa kutokana na mashaka kwamba Marekani inaweka msisitizo zaidi kwenye usalama wa Israel pekee bila kujali matakwa ya Wapalestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *