London, England. Akiwa amerejea England kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Real Madrid, Jude Bellingham alitarajiwa kuvutia macho ya kocha Thomas Tuchel kwenye mechi dhidi ya Liverpool, lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia.
Tuchel hakuhudhuria kabisa Anfield, wala msaidizi wake Anthony Barry jambo lililoongeza hofu kuwa hataitwa tena kwenye kikosi kijacho cha England wiki ijayo.
Kwa bahati mbaya zaidi, Bellingham hakucheza vizuri; alifunikwa kabisa, Real Madrid ikipoteza 1–0, na akashindwa kuonyesha makali yake dhidi ya Majogoo hao wa Anfield.
Tuchel bado anamnyima nafasi
Tangu kuchukua mikoba ya Gareth Southgate, Tuchel amekuwa akionyesha kuwa anaweza kujenga timu imara bila Bellingham.
England imekuwa ikiibuka na ushindi mnono kwenye michezo ya kufuzu ikiwemo kuifunga Latvia 5–0, Wales 3–0, Serbia 5–0, na Andorra 2–0.
Kwa matokeo hayo, Tuchel anaonekana kuendelea kuwaamini wachezaji waliocheza vizuri Septemba, badala ya kumpa Bellingham nafasi.
Tuchel amesema:
“Hakuna aliyekosea. Hii si adhabu. Bellingham ni mchezaji mkubwa, muhimu, lakini nina imani na kikosi kilichofanya kazi vizuri.”
Lakini wachambuzi wanasema huu ni mchezo wa nguvu wa Tuchel akionyesha kuwa hakuna mchezaji, hata nyota wa Real Madrid, aliye juu ya timu.
Kwenye mashindano ya Euro yaliyopita, alijipa umaarufu kwa jeuri yake alipofunga dhidi ya Slovakia na kuuliza, “Who else?” (Nani mwingine?). Sasa, jibu la Tuchel linaonekana kuwa: “Wengine wapo.”
Ikiwa ataendelea kupuuzwa kwenye kambi za kimataifa zinazofuata, kuna hatari kubwa kwamba England inaweza kuelekea Kombe la Dunia bila yeye jambo ambalo litakuwa la kushangaza kwa mchezaji ambaye zamani alionekana kuwa uso mpya wa taifa hilo.