
Video za kushtua zimeibuka zikimuonesha kamanda wa kikundi cha waasi wa RSF nchini Sudan akijigamba kwa kuwaua binafsi zaidi ya raia 2,000 wakati wa utekaji wa mji wa El Fasher ulioko Darfur.
Video zinazozunguka mitandaoni zinaonesha al-Fateh Abdullah Idris, anayejulikana sana kwa jina la kivita Abu Lulu, akiwaua raia wasio na silaha kwa risasi za karibu, jambo lililompa lakabu “Mchinjaji wa El-Fasher” na kumfanya kuwa ishara ya mauaji ya halaiki katika eneo hilo.
Abu Lulu, mmoja wa makamanda wa RSF wanaoogopwa sana, alipata umaarufu kwa kuonekana katika video kadhaa akisimamia mauaji ya mateka na raia. Hata hivyo, ukatili wa hivi karibuni huko El Fasher, ambako alikiri kuwaua maelfu kwa mikono yake na kurekodi mauaji ya halaiki, unaonesha kiwango chake cha juu cha ukatili.
Katika matangazo ya moja kwa moja ya TikTok yaliyoogofya, Abu Lulu alijigamba: “Nilitaka kuua 2,000, lakini nina hakika idadi ilizidi 2,000. Nilipoteza hesabu, lakini nitaanza tena kutoka sifuri.”
RSF, chini ya uongozi wa Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, iliteka El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini wiki iliyopita, katika mojawapo ya vipindi vya umwagaji damu zaidi vya vita vinavyoendelea kati ya kikundi hicho cha waasi na jeshi la Sudan, vilivyoanza Aprili 2023 na kusababisha maangamizi makubwa nchini Sudan.
Hayo yanajiri wakati Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeongeza juhudi za kukusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanyika wakati wa utekaji wa El Fasher na RSF.
ICC inachukua hatua za haraka kukusanya na kuhifadhi ushahidi kwa ajili ya mashitaka yanayoweza kufunguliwa, huku wasiwasi wa kimataifa ukiongezeka kuhusu janga la kibinadamu linalozidi kuwa mbaya nchini Sudan.
Mji wa El Fasher umetekwa na RSF huku dunia ikiangazia nafasi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika umwagaji damu huo.
UAE imebainika kuwa kama mfadhili mkuu wa kimataifa wa kikundi cha waasi wa RSF wa Sudan, ikiwapa msaada wa kijeshi na kifedha unaohitajika kwa kampeni ya mauaji ya kimbari.
Msaada huo unaonekana si wa kimya kimya bali ni mkakati wa makusudi na wa moja kwa moja kufanikisha malengo ya kisiasa na kiuchumi ya UAE katika eneo la Pembe ya Afrika, huku nchi hiyo ya Kiarabu ikikodolea macho ya tamaa dhahabu ya Sudan na fukwe zake zake za Bahari Nyekundu.