Dar es Salaam. Msanii chipukizi wa muziki nchini, Diameter Pallet ambaye anatamba na wimbo ‘Kidampa’, ameweka wazi namna wimbo huo unavyogusa maisha yake.

Akizungumza na Mwanachi amesema Kidampa ndio wimbo wake wa kwanza kufanya vizuri zaidi na unahusu stori ya kweli ambayo iliwahi kumtokea hapo nyuma.

“Hii ni project yangu ya kwanza ambayo imefanya vizuri zaidi. Kiukweli kipindi naandika huu wimbo nilijiandikia mimi kabisa. Maana ni stori ya kweli inayonihusu, lakini nashukuru Mungu baada ya wimbo kutoka nikaona sio mimi pekeyangu nilikuwa nateswa. Kumbe kuna watu wengi wanapitia hali kama yangu,” amesema.

Hatahivyo amesema yule mwanamke anayeonekana kwenye kipande cha video iliyosambaa na kupaisha zaidi wimbo huo ni shabiki tu, hawakuwahi kufahamiana.

“Nilikuwa sifahamiani nae. Sasahivi ni mtu wangu wa karibu. Nakumbuka ilikuwa kwenye shoo director wangu akaniambia anataka challenge zetu, siku hiyo zihusu mashabiki wanaoimba na sisi. Baada ya kumaliza shoo tumerudi nyumbani akanionesha video ya huyo dada Frola.

“Nikamwambia hii video nzuri inaweza ikasaidia kwenye promosheni. Tukaipandisha mtandaoni baada ya masaa mawili ikaanza kuleta majibu na challenge zikaanza kumwagika kwa wingi,” amesema.

Amesema licha ya Frola kuwa miongoni mwa watu waliosababisha ‘Kidampa’ kusambaa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, alikataa kabisa malipo ya shukurani.

“Nashukuru Mungu Frola ni moja ya watu wamesaidia sana huu wimbo kwenda. Tulipanga kumtafuta lakini bahati nzuri yeye mwenyewe akanicheki. Tukakutana nikataka kumpa hela akaikataa, video imempa vitu vingi,” amesema.

Aidha amesema amejipanga vizuri ana nyimbo nyingi kali zaidi ya ‘Kidampa’ ambazo anatarajia kuachia hivi karibuni.

“Kiukweli nimejipanga vyakutosha.  Hata kipindi tunaachia ‘Kidampa’ tuliachia orodha ya nyimbo zetu. Jinsi tulivyozipanga ni kwa ukali, iliyo juu ya ‘Kidampa’ ni kali kuliko ‘Kidampa’ yenyewe na baada ya hiyo ipo kali zaidi, tutegemee tuu makubwa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *