Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 90 ya nchi zilizochunguzwa, nchi 161 kati ya 176 zinatarajiwa kushuhudia kupungua kwa mavuno ya mazao muhimu ya chakula ifikapo mwishoni mwa karne hii, hata baada ya kuzingatia mbinu na mikakati ambayo wakulima wanaweza kutumia kukabiliana na hali hiyo.

“Mabadiliko ya tabianchi si changamoto ya kimazingira pekee ni janga kubwa la maendeleo, amesema Pedro Conceição, Mkurugenzi wa Ofisi ya Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya UNDP. “Mavuno bora ya kilimo ni muhimu si kwa usalama wa chakula tu, bali pia kwa ustawi wa maisha na maendeleo ya kiuchumi. Tishio kwa mavuno ya kilimo na pia ni tishio kwa maendeleo ya binadamu leo na kesho,” ameongeza.

Takwimu zenye wigo mpana wa kimataifa

Utafiti mpya uliotokana na Hultgren et al. (2025) umeunganisha viashiria vya tabianchi na mavuno ya mazao sita makuu duniani mahindi, mpunga, ngano, soya, muhogo na mtama. Utafiti huo umeangalia mikakati ya wakulima chini ya hali mbili tofauti za mabadiliko ya tabianchi: moja ikizingatia upunguzaji wa wastani wa hewa ukaa, na nyingine ikiwa na uzalishaji mkubwa wa hewa chafu.

Takwimu hizo zimepangwa kwa vipindi vitatu vya muda: muda mfupi (2020–2039), katikati ya karne (2040–2059), na mwishoni mwa karne (2080–2099). Zinaonesha mabadiliko ya mavuno katika idadi ya maeneo madogo zaidi ya 19,000 katika nchi zaidi ya 100, zikitoa taswira ya kina na ya ushahidi kuhusu jinsi joto na viwango vya utoaji wa hewa chafu vinavyoweza kubadilisha mifumo ya chakula na maendeleo ya binadamu duniani.

Nchi zenye maendeleo duni ndizo zinazoathirika zaidi

Kwa mujibu wa takwimu hizo, nchi zenye kiwango cha chini cha Maendeleo ya Binadamu (HDI) ndizo zitakazokumbwa na hasara kubwa zaidi. Mavuno ya mazao katika nchi hizi yanatarajiwa kupungua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 25 hadi 30 ifikapo mwisho wa karne hii, endapo uzalishaji wa hewa chafu utaendelea kuwa mkubwa.

Sehemu nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia zimeainishwa kuwa katika hatari zaidi, kutokana na utegemezi mkubwa wa mvua badala ya umwagiliaji na upungufu wa rasilimali za kukabiliana na mabadiliko hayo.

Wakati huohuo, hata mikoa mikubwa ya uzalishaji wa chakula duniani ikijumuisha wazalishaji wakuu wa ngano na soya haitasalimika. Chini ya ongezeko kubwa la joto, mavuno katika maeneo haya yanaweza kushuka hadi kwa kiwango cha asilimia 40, hali inayoweza kusababisha changamoto katika bei za chakula, biashara ya kimataifa na uthabiti wa kiuchumi duniani.

Wito wa haraka kwa hatua za usawa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Matokeo haya yanathibitisha ujumbe wa Tamko la Belém kuhusu Njaa, Umaskini na Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Zilizolenga Maendeleo ya Binadamu, lililotolewa kuelekea Mkutano kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP30 nchini Brazil. Tamko hilo linasisitiza kuwa mifumo ya chakula na usawa vinapaswa kuwa kiini cha mikakati ya dunia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti pia umeonesha kuwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kuna matokeo chanya. Nchi zinazopunguza uzalishaji hadi viwango vya wastani zinatarajiwa kupoteza chini ya nusu ya mavuno ikilinganishwa na nchi zilizo na uzalishaji mkubwa ifikapo mwaka 2100. Hali hii inadhihirika katika nchi tajiri na maskini kwa usawa, ikionyesha kuwa hatua thabiti za kupunguza na kuhimili mabadiliko ya tabianchi zinaweza kupunguza athari kwa watu na jamii kwa kiasi kikubwa.

“Njia ya kuelekea mustakabali endelevu na wa haki ni kupitia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazozingatia maendeleo ya kibinadamu,” ameongeza Conceição. “Kuhakikisha kila mtu anapata chakula cha kutosha, chenye lishe na cha uhakika si suala la kuishi tu ni msingi wa heshima na maendeleo ya binadamu.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *