Liverpool, England. Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsène Wenger amefichua kwamba Liverpool ilivuruga mfumo wake wa kiungo ambao ulikuwa unafanya kazi vizuri kabla ya kufanya mabadiliko ya kutumia mfumo mwingine.
Ili kumpa Florian Wirtz nafasi ya kucheza namba 10, walimtoa Dominik Szoboszlai kwenye eneo la kati, na matokeo yake yakawa mabaya timu ikashinda mechi moja pekee kati ya saba.
Majogoo hao wa Anfield waliipiku Bayern Munich kwa kumsajili kiungo huyo wa Ujerumani kwa dau la paundi milioni 116 sawa na Sh400 bilioni za Kitanzania lakini sharti la mchezaji kabla ya kusajiliwa lilikuwa ni kucheza namba 10, si pembeni.
Wenger amesema:
“Liverpool walikubali kumchezesha Wirtz namba 10, wakaharibu ubora wa kiungo chao cha Gravenberch, Mac Allister na Szoboszlai. Walipomrudisha Szoboszlai, wakarudisha uthabiti wao.”
Ndiyo maana kwenye mechi dhidi ya Aston Villa na Real Madrid, kocha Arne Slot alirudisha mfumo wa zamani Wirtz akacheza pembeni badala ya katikati, na ghafla Liverpool wakashinda mechi mbili mfululizo bila kuruhusu bao.
Wenger anasema sasa Slot amemwambia Wirtz atacheza pembeni kama anataka kuendelea kucheza, ili kulinda uimara wa timu. Hata hivyo, hilo linaweza kumuweka Cody Gakpo katika hatari ya kupoteza namba, kwani ndiye aliyekuwa akicheza winga ya kushoto.
Kwa sasa, macho yote yapo kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Manchester City ambapo Slot atahitaji nguvu kubwa katikati kuzuia mashambulizi ya Erling Haaland, ambaye ana mabao 17 katika mechi 13 tu!