Mshambuliaji wa Atalanta, Ademola Lookman, alilazimika kushikiliwa na wachezaji wenzake baada ya kutaka kumvamia kocha wake Ivan Juric katika vurugu zilizotokea muda mfupi baada ya yeye kutolewa uwanjani jana usiku.

Tukio hilo lilitokea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa kwenye Uwanja wa Vélodrome, ambapo Atalanta iliibuka na ushindi wa 0-1 ugenini dhidi ya Marseille ya Ufaransa.

Dakika ya 75, huku mchezo ukiwa bado 0-0, Juric alimtoa Lookman, jambo lililomkera mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria. Alipotoka uwanjani, walianza kubishana kwa maneno na kocha wake kabla hali haijachafuka zaidi.

Kwa mujibu wa mashuhuda, Juric alimvuta Lookman kwa hasira, jambo lililomfanya mshambuliaji huyo ajibu kwa ghadhabu, na ndipo CEO wa klabu Luca Percassi pamoja na nahodha Marten de Roon wakaingilia kati kumtuliza.

Baada ya mchezo, Juric alionekana kumfuata tena Lookman na kuzungumza naye, ingawa haijulikani kama walikuwa wanamaliza tofauti au wanaendeleza ubishi. Siyo mara ya kwanza Lookman kugombana na makocha

Lookman, mwenye umri wa miaka 28, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Atalanta tangu aliposajiliwa mwaka 2022, akiwa amefunga mabao 40 katika mechi 99 na kuongoza timu kushinda taji la Europa League msimu wa 2023-2024.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kuhusishwa na utata ndani ya klabu hiyo. Mwaka huu, aliingia kwenye mgogoro wa wazi na kocha wa zamani Gian Piero Gasperini, baada ya kocha huyo kumuita “miongoni mwa wapigaji penalti wabaya zaidi” kufuatia kipigo dhidi ya Club Brugge.

Lookman alijibu kupitia mitandao ya kijamii akisema:

“Kutajwa hadharani kwa namna hii kunaniumiza na kunavunja heshima, hasa nikizingatia bidii na kujituma kwangu kila siku kwa ajili ya timu na mashabiki wa Bergamo.”

Baada ya hapo, alijaribu kulazimisha kuondoka msimu wa joto, huku Inter Milan ikitoa ofa ya pauni milioni 32, na klabu kama PSG pia zikionesha nia. Lakini uhamisho wake ukazimwa na Atalanta.

Hali sasa yachafuka tena

Lookman alirejea na kuanza msimu huu vizuri, lakini tukio hili jipya linaibua maswali kuhusu mustakabali wake. Wachambuzi nchini Italia wanasema dirisha la Januari linaweza kuwa suluhisho pekee kama hali haitatulia.

Mchezaji huyo, aliyewahi kuichezea England katika ngazi za vijana kabla ya kuchagua Nigeria kwa timu ya taifa, alianza soka la kulipwa Charlton Athletic, kisha akaenda Everton, kabla ya kuhamia RB Leipzig, Fulham, na Leicester City kwa mkopo.

Atalanta ilimnunua kwa pauni milioni 13 dili ambalo lilionekana kuwa kubwa, lakini sasa linaweza kuisha kwa mgogoro kama hatapatana na Juric.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *