Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesifu kusimama kidete kwa nchi dhidi ya uvamizi wa hivi karibuni wa siku 12 wa Marekani na Israel, akisema kusimama kidete huko kulimlazimisha adui aliyetaka Iran ijisalimishe bila masharti, kuomba kusitishwa mapigano bila masharti.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Utawala katika mkoa wa Hamedan jioni ya jana Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alitangaza kwamba adui alishindwa kabisa kufikia malengo yake yote katika vita vya siku 12.

Araqchi ameeleza kwa undani makosa yaliyofanywa na adui katika kuanzisha vita hivyo, akibainisha dhana yao kwamba Iran ingesalimu amri haraka kutokana na mashambulizi ya ghafla.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ameashiria siku za mwanzo za vita, walipotuma ujumbe wakitaka Iran kuingia kwenye mazungumzo ya kujisalimisha, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akisisitiza kauli yake maarufu ya kuitaka Iran “ijisalimishe bila masharti” katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii.

“Katika siku za mwanzo kabisa za vita, Rais wa Marekani alituma ujumbe wenye maneno matatu kwenye Twitter: “Kujisalimisha bila masharti.” Lengo lao la kuanzisha vita lilikuwa mashambulizi ya ghafla na ya kushtukiza, na walidhani kwamba Iran ingeinua mikono juu na kujisalimisha ndani ya siku 2-3. Hata hivyo, hili halikufanikiwa kutokana na hekima ya Kiongozi Mkuu, kuteuliwa haraka makamanda wapya wa jeshi, ukarabati wa vikosi vya jeshi, na ushiriki mkubwa wa serikali katika usimamizi wa migogoro na kukidhi mahitaji ya nchi”, amesema Waziri wa Mambo ya Nje.

Amesema “Majibu sahihi, ya wakati, yenye nguvu, na ya kina ya vikosi vyetu vya jeshi kwa uchokozi wa adui pia yalikuwa muhimu sana katika kushindwa kwao.”

Akizungumzia madai ya nchi za Magharibi, Araqchi amesema: “Niliwaambia wakuu wa nchi hizo wakati wa mkutano wangu na wao kwamba wengi walidai anga la Iran ilikuwa mikononi mwa ndege za kivita za Israel wakati wa vita vya siku 12, lakini hawajataja ukweli kwamba anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilitawaliwa na makombora ya Iran, na kwamba licha ya ulinzi wa anga wa tabaka nyingi kwa msaada wa Marekani na nchi za Ulaya, hawakuweza kuzuia makombora ya Iran.”

“Makombora yetu, kwa mara ya kwanza katika vita, yalipiga maeneo ya adui kwa usahihi na kwa uthabiti kila siku,” amesema Araqchi na kuongeza kuwa: sambamba na hekima ya Kiongozi Mkuu, nguvu ya vikosi vya jeshi, na juhudi za serikali na timu ya diplomasia, umoja wa kitaifa wa wananchi na muqawama pia vilikuwa na umuhimu mkubwa katika ushindi dhidi ya adui katika vita vya siku 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *