Mawaziri wa utawala katili wa Israel wameonyesha ghadhabu kufuatia kuchaguliwa kwa Zohran Mamdani kuwa meya wa jiji la New York nchini Marekani, wakimshambulia kwa tuhuma mbalimbali.

Mamdani, ambaye ni Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa kuongoza jiji kubwa zaidi nchini Marekani, amewahi kulaani operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza kama mauaji ya kimbari, na ameahidi kuheshimu waranti wa kimataifa wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Waziri wa Usalama wa Taifa wa mrengo wa kulia wa Israel, Itamar Ben-Gvir, amedai kuwa ushindi wa Mamdani ni ishara kwamba “chuki dhidi ya Wayahudi imeishinda busara,” huku akimtaja meya huyo aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Democrat kuwa “mfuasi wa Hamas.” Ben-Gvir alidai kuwa Mamdani anahadaa anaposema Israel imetekeleza mauaji ya kimbari Gaza.

Kinara wa upinzani katika utawala haramu wa Israel, Avigdor Liberman, naye pia amekariri msimamo huo, akimtaja Mamdani kama “mbaguzi na Mwislamu mwenye misimamo mikali.” Liberman amewataka Wayahudi wa New York wahamie Israel, akidai jiji limechagua mtu ambaye ni “nembo ya jihad.”

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Sharren Haskel, pia alidai kwamba mitazamo ya Mamdani inaleta hatari kwa jamii ya Kiyahudi ya New York.

Kauli za kumpinga Mamdani zilizotolewa na wakuu wa utawala haramu wa Israel zinatofautiana na zile za Wayahudi wenye misimamo ya wastani ambao wamemuunga mkono meya huyo mpya wa New York.

Ushindi wa Mamdani ni mabadiliko ya kihistoria kutoka katika utamaduni wa miongo mingi wa mameya wa New York waliokuwa wakiunga mkono utawala dhalimu wa Israel. Matokeo hayo yanakuja wakati ambapo kuna ongezeko la upinzani duniani dhidi ya kampeni ya kijeshi ya Israel huko Gaza, iliyoendelea kwa zaidi ya miaka miwili.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, kauli za maafisa wa Israel zinaonyesha kushadidi kwa wasiwasi mjini Tel Aviv, hasa kwa kuwa Wamarekani—hasa vijana—wanapinga hatua za Israel dhidi ya Wapalestina.

Mamdani, ambaye amekuwa mtetezi wa haki ya Wapalestina kujiamulia mambo yao, amekataa tuhuma za chuki dhidi ya Wayahudi, na ameahidi kupambana na chuki yoyote.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *