
Rais wa zamani wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz, ameshindwa katika rufaa yake ya mwisho aliyokata ya kupinga kifungo cha miaka 15 jela alichohukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi alipokuwa madarakani. Mahakama ya Juu ya Mauritania imeidhinisha hukumu hiyo.
Hapo awali mnamo mwaka 2023, Abdel Aziz alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kujilimbikizia mali na mtaji wenye thamani ya dola milioni 70 kwa njia za haramu. Mawakili wake walidai kwamba kesi hiyo ilichochewa na utashi wa kisiasa, lakini rufaa yake ya kwanza aliyokata kupinga hukumu aliyopewa ilikataliwa Mei 2025 na kifungo chake kiliongezeka kwa miaka 10 na kuwa miaka 15.
Baada ya kutwaa madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2008, Abdel Aziz alichaguliwa mara mbili kuwa rais na alihudumu kuanzia mwaka 2009 hadi 2019 alipong’atuka madarakani kwa kumalizika mihula yake ya uongozi.
Mnamo mwaka 2021, rais huyo wa zamani wa Mauritania mwenye umri wa miaka 68, alishtakiwa kwa kujitajirisha kinyume cha sheria, kutumia vibaya madaraka, na kuhusika na utakatishaji pesa kwa ushirikiano na watu wengine 10 mashuhuri, wakiwemo mawaziri wakuu wawili wa zamani.
Tangu alipohukumiwa, Mohamed Ould Abdel Aziz amepokonywa mali zake na haki za kiraia…/