
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamesema Jumatano kuwa yana wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za kuongezeka kwa ukatili na madhila dhidi ya raia wanaokimbia mji wa El Fasher, Sudan.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema imekuwa ikipokea taarifa nyingi zinazoongezeka kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za raia, huku mapigano yakiendelea katika jimbo la Darfur Kaskazini.
Ofisi hiyo imesema uchambuzi wa picha za setilaiti umebaini kuwepo kwa angalau makaburi mawili ya pamoja karibu na msikiti na hospitali ya zamani ya watoto, pamoja na maeneo kadhaa yanayoonyesha dalili za kutupwa kwa miili ya watu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limeripoti kuwa wanawake na wasichana wanakabiliwa na kubakwa, kutekwa, na aina nyingine kali za ukatili wanapokimbia El Fasher.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa kufikia Jumanne, karibu watu 82,000 walikuwa wamekimbia El Fasher na maeneo jirani tangu mji huo ulipotekwa na waasi wa kundi la RSF mnamo Oktoba 26.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeripoti kuwa nchi jirani upande wa magharibi, Chad, imekuwa makimbilio muhimu kwa wanaokimbia machafuko ya Sudan, na sasa inawahifadhi takriban wakimbizi milioni 1.4, wengi wao kutoka Darfur.
Mji wa El Fasher umetekwa na RSF, huku dunia ikiangazia nafasi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika umwagaji damu huo.
UAE imebainika kuwa mfadhili mkuu wa kimataifa wa kikundi cha waasi wa RSF wa Sudan, ikiwapa msaada wa kijeshi na kifedha unaohitajika kwa kampeni ya mauaji ya kimbari.
Msaada huo unaonekana si wa kimya kimya, bali ni mkakati wa makusudi na wa moja kwa moja kufanikisha malengo ya kisiasa na kiuchumi ya UAE katika eneo la Pembe ya Afrika, huku nchi hiyo ya Kiarabu ikikodolea macho kwa tamaa dhahabu ya Sudan, ardhi ya kilimo, na fukwe zake za Bahari Nyekundu.