Waliokuwa wapiganaji wa Mau Mau nchini Kenya kutoka Kaunti ya Meru wameishtaki Serikali, wakitaka iwalipe fidia ya shilingi bilioni 10 kwa vitendo vya ukiukaji wa haki walivyotendewa baada ya nchi hiyo kupata uhuru.

Wakili Tom Macharia, anayewakilisha walalamikaji hao, ameiambia mahakama kwamba wateja wake wanataka pesa hizo zilizopasa kutolewa kupitia Hazina ya Haki iliyopendekezwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo mwaka 2015.

“Wakati wa hotuba yake kwa taifa mnamo 2015, Rais Kenyatta aliomba msamaha kwa wapigania uhuru wote. Aliagiza kuundwa kwa Hazina ya Haki na kanuni kuhusu kuundwa kwake zilitayarishwa na Mwanasheria Mkuu,” wakili Macharia ameiambia mahakama.

Mashujaa hao wa Mau Mau pia wanaitaka mahakama itoe agizo la utekelezaji wa mapendekezo ya Tume kuhusu Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ili kutoa haki na maridhiano kwa wapiganaji wa Mau Mau na familia zao.

Wameishtaki serikali kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu.

Mahakama Kuu iliwasilisha kesi hiyo kwa Jaji Mkuu ili ateue jopo la majaji kuisikiliza na kutoa uamuzi.

Katika agizo lake, Jaji Heston Nyaga amesema, kesi hiyo inaibua masuala mazito ya kikatiba “yanayoathiri maelfu ya wapigania uhuru nchini Kenya na hivyo inafaa kusikilizwa na jopo la majaji.”

Jaji Nyaga ameamuru walalamikaji kuweka tangazo hilo katika sehemu ya gazeti ambapo litaonekana wazi, ndani ya siku 21. Aidha, amewaagiza wahusika kujiwasilisha kortini kwa ajili ya kusikilizwa kesi hiyo siku 21 baada ya tangazo lake kuchapishwa magazetini.

“Maagizo zaidi yatasubiriwa kutoka kwa afisi ya Jaji Mkuu. Kesi hiyo itatajwa na maagizo kutolewa mnamo Februari 9, 2026,” ameamuru Jaji Nyaga.

Kesi hiyo imewasilishwa na jumla ya waliokuwa wapigania uhuru 30 na jamaa za mashujaa wa Mau Mau na shirika lisilo la kiserikali la African Centre for Corrective and Preventive Action (ACCPA)…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *