
Shirika la habari la Reuters limenukuu chanzo cha kuaminika ambacho hakikutaka kitajwe na kutangaza kwamba serikali ya Trump inapitia ombi la Saudi Arabia la kununua ndege 48 za kivita za kisasa za F-35, mpango wa mabilioni ya dola ambao umeondoa moja ya vikwazo vikubwa katika Wizara ya Vita ya Marekani na ambao unajadiliwa sanjari na ziara ijayo ya Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman huko nchini Marekani.
Ripoti ya Reuters imesema, uuzaji huo tarajiwa ni mabadiliko makubwa katika sera za Washington ambayo yanaweza kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi katika Mashariki ya Kati na kutoa changamoto kwa kauli ya Marekani ya kudumisha uwezo wa juu zaidi wa kijeshi wa Israel, ambayo ndiyo pekee inayomiliki ndege hizo za kivita za kisasa katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa duru za kuaminika, Saudi Arabia iliwasilisha ombi lake la moja kwa moja kwa Rais wa Marekani Donald Trump mapema mwaka huu, na kwa muda mrefu imekuwa na hamu ya kuwa na ndege za kivita zilizotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin.
Ripoti ya Reuters imeongeza kuwa, hivi sasa Pentagon inachunguza uwezekano wa kuuza ndege 48 kati ya ndege hizo za kisasa.
Kwa mujibu wa duru za Washington uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo bado haujafanywa na kwamba hatua zaidi zinahitajika, ikiwa ni pamoja na idhini ya baraza la mawaziri, sahihi ya Trump na utoaji taarifa kwa Bunge la Kongresi.
Vyombo vya habari vya lugha ya Kiarabu viliripoti hapo kabla kwamba Mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman atakutana na Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa ziara yake mjini Washington itakayofanyika Novemba 18, huku nchi hizo mbili zikitarajia kusaini makubaliano makubwa.
Ziara ya Bin Salman huko Washington itafanyika wakati Trump anajaribu kuihimiza Saudia ijiunge na mpango wa kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa kizayuni wa Israel unaojulikana kama Mkataba ya Abraham.
Mkataba huo ulitiwa saini kwa mara ya kwanza mwaka 2020 kati ya Israel na Muungano wa Falme za Kiarabu UAE, Bahrain, Sudan na Morocco, ambapo kwa hatua hiyo, nchi hizo nne za Kiarabu na Kiislamu zikaanzisha rasmi uhusiano wa kawaida na utawala huo wa kizayuni. Saudi Arabia imeonyesha kusita kujiunga na makubaliano hayo ikidai kwamba hakuna hatua za vitendo zilizochukuliwa ili kuanzisha nchi dola ya Palestina…/