Sekta ya chai nchini imeendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi, ikichangia ajira, pato la Taifa na kuinua maisha ya maelfu ya wakulima vijijini. Lakini pia chai ni mojawapo ya mazao ya biashara yanayoiingizia nchi fedha za kigeni.
Sekta hii imekuwa ikipata nguvu mpya miaka ya karibuni baada ya uboreshaji wa sera za uwekezaji, uboreshaji wa sekta ya kilimo, uwekezaji katika viwanda vya usindikaji na juhudi za kujenga soko la kimataifa lenye thamani zaidi.
Kilimo cha Chai ambacho awali ilikuwa ni shughuli ambayo wakulima wanaifanya kwa ajili ya kukidhi maisha yao ya kawaida, sasa ina fursa nyingi ikiwemo kuongeza thamani, kuunganisha wakulima wadogo kwenye minyororo ya thamani ya zao hilo na kuboresha uzalishaji kupitia teknolojia na miundombinu ya umwagiliaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bi. Beatrice Banzi
Hilo limesaidia kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya chai sokoni msimu wa hivi karibuni. Serikali kupitia Bodi ya Chai Tanzania na wadau wamechukua hatua za kuwekeza katika kurejesha viwanda vilivyokuwa wa vimeacha kuzalisha na kujenga vipya vya kuchakata ili kuongeza uwezo wa kusindika majani ya chai na kuzalisha “made tea” yenye ubora wa kuuza nje. Hatua hizi zimechangia kupanua soko la kuuza nje na kuongeza mapato ya sekta.
Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bi. Beatrice Banzi alieleza maendeleo ya sekta hiyo, mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mikakati mipya inayolenga kuifanya chai ya Tanzania kuwa miongoni mwa chai bora zaidi duniani.
Sekta ya chai Tanzania na maendeleo yake
Bi. Beatrice anasema sekta ya chai Tanzania imepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Kwa sasa Tanzania inazalisha takribani tani 22,000 kwa mwaka lakini uwezo halisi wa kuzalisha ni tani 60,000 japokuwa kiasi kikubwa (asilimia zaidi ya 90) kinaenda katika masoko ya nje kama Pakistan, Japani, China, Qatar, Oman, UAE na kwingineko, jambo ambalo linasababishwa na mwamko wa Watanzania katika matumizi ya chai na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kinywaji hicho.
“Watanzania wengi hawana mwamko wa kutumia chai. Wengi wetu tunatumia chai kwa mazoea jambo ambalo sio sahihi kwani chai ni kinywaji chenye faida nyingi za kiafya mwilini ikiwemo kuboresha mzunguko wa damu, kukuepusha na magonjwa mbalimbali, kuupa mwili nguvu nk. Hivyo tunapaswa kutumia chai mara kwa mara kama tunavyotumia maji,” anasema Bi. Beatrice.
Anasema sekta ya chai imekuwa ikiimarika kutokana na jitihada za Serikali, taasisi za utafiti, na mashirika ya maendeleo yaliyowekeza katika kuboresha mbegu, kuongeza tija na kuimarisha usimamizi wa ubora.
“Wakulima wetu wameanza kuelewa thamani ya ubora. Tunashuhudia ongezeko la matumizi ya mbegu bora na mbolea za kisasa, sambamba na elimu juu ya usimamizi bora wa mashamba. Lakini pia Serikali imefanya kazi kubwa katika kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima,” anaeleza Bi. Beatrice.
Juhudi za Serikali kufungua fursa za masoko na uwekezaji
Akizungumzia mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Bi. Beatrice anasema kuwa Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Rais Samia amekuwa kinara katika kufungua milango ya masoko mapya kupitia diplomasia ya kiuchumi. Kupitia safari na mikutano yake na viongozi wa mataifa mbalimbali, chai ya Tanzania imepata mwanga mpya katika soko la dunia,” anasema Bi. Beatrice.
Anaongeza kuwa Serikali imewekeza pia katika miundombinu ya barabara na umeme vijijini, jambo lililosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa chai kutoka mashambani hadi viwandani.
“Uwekezaji wa Serikali katika miundombinu umeongeza ushindani wa wakulima wetu. Hii ni sehemu ya ajenda pana ya Rais Samia ya kufungua fursa za kiuchumi vijijini,” anaeleza.
Anasema kupitia juhudi za Rais Samia katika kufungua milango, Bodi ya Chai imepata fursa ya kuhudhuria katika mataifa mbalimbali na kuonyesha namna chai ya Tanzania ilivyokuwa bora na hatua inayopitia katika uwekezaji wake.
“Ziara hizo zimetusaidia kufungua fursa mpya za masoko. Kwa mfano ziara tuliyoifanya Japan imewezesha wawekezaji wa Japan kufanya ziara maalumu nchini kwa ajili ya kuja kuona fursa zilizopo na wameshaanza mchakato wa kuwekeza katika sekta ya chai,” anasema Bi. Beatrice.
Bodi ya Chai Tanzania: Kinara wa ukuzaji na uongezaji tija ya sekta ya chai
Bodi ya Chai Tanzania imekuwa kiungo muhimu kati ya wakulima, wazalishaji na soko. Bi. Beatrice anasema kuwa bodi hiyo imeweka mikakati ya kuimarisha uzalishaji kupitia mafunzo, utafiti, na uwekezaji katika teknolojia.
“Tumeanzisha mpango wa kitaifa wa kuongeza tija unaojumuisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha chai, matumizi sahihi ya pembejeo na utunzaji wa mazingira. Pia tumeanzisha mashamba ya mfano,” anasema.
Kwa mujibu Bi. Beatrice hatua hizo zimeongeza uzalishaji kwa zaidi katika miaka mitatu iliyopita, huku ubora wa majani mabichi ukiongezeka kwa kiwango kikubwa. Mbali na hilo bodi pia imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi katika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua.
Mkulima akifurahia mavuno ya chai.
“Tumekuwa na ushirikiano mzuri na taasisi mbalimbali hususani zilizpo chini ya Wizara ya Kilimo ikiwemo wakala wa mbegu, taasisi za utafiti wa kilimo pamoja na nyingine chini ya Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ikiwemo Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA), TANTRADE, TISEZA na KOTRA. Ushirikiano huu umesaidia kufungua fursa za masoko ya chai ndani na nje ya Tanzania,” anasema Bi. Beatrice.
Mnada wa Chai: Mkakati mpya wa kuboresha bei na kuongeza uwazi wa mauzo ya chai
Moja ya mafanikio makubwa ya sekta ya chai Tanzania ni kuanzishwa kwa mnada wa chai jijini Dar es Salaam mwaka 2023 ambao unaendeshwa na Bodi ya Chai Tanzania kwa kushirikiana na wadau kila siku ya Jumatatu. Mnada huo unafanyika katika ghala la bodi hiyo lililopo eneo la Kipawa.
“Kabla ya hapo, chai nyingi za Tanzania ziliuzwa kupitia mnada wa Mombasa. Hii ilipunguza udhibiti na uwazi kwa wazalishaji wetu. Lakini tangu tuanzishe mnada wetu, wakulima wameanza kuona faida moja kwa moja,” anasema Bi. Beatrice.
Ameeleza kuwa mnada huo umeongeza ushindani na uwazi katika bei, ambapo wakulima sasa wanapata taarifa kamili kuhusu thamani ya zao lao sokoni.
“Kupitia mfumo wa kidijitali wa minada, bei zinatangazwa hadharani na wakulima wanaweza kufuatilia mwenendo wa soko kwa wakati halisi. Hii imeongeza imani, mapato na kuimarisha utendaji wa sekta kwa ujumla,” anaeleza Bi. Beatrice.
Ubora na thamani ya chai ya Tanzania katika soko la dunia yapaa
Ubora wa chai ya Tanzania umeendelea kuvutia wanunuzi wa kimataifa. Bi. Beatrice anasema chai ya Tanzania ina ladha ya kipekee inayotambulika duniani.
Moja ya mashamba ya chai nchini likiwa katika muonekano wa kuvutia.
“Chai yetu ina harufu nzuri na ladha laini yenye asili ya udongo na mazingira ya asili ya kitanzania. Hii ndiyo inayoifanya iwe tofauti na chai kutoka maeneo mengine,” anaeleza.
Anasema kuwa bodi imeendelea kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine kuhakikisha viwango vya ubora vinafuatwa kuanzia shambani hadi sokoni.
“Kila mzigo wa chai unaopitia minadani na kusafirishwa nje hupimwa ubora wake. Tunataka chai ya Tanzania iwe nembo ya ubora Afrika Mashariki na duniani,” anasema Bi. Beatrice.
Anasema chai ya Tanzania sasa imekuwa na thamani kubwa katika masoko mbalimbali duniani ambapo kwa wastani inauzwa kuanzia Dola za Marekani 1.55 hadi 60 kwa kilo kutegemeana na aina ya chai. Hili ni jambo la kujivunia kwani sisi ni moja ya nchi ambazo chai yetu ina ubora wa kipekee na thamani kubwa sokoni.
Uwekezaji katika teknolojia na mifumo ya kidijitali waongeza ufanisi wa sekta ya chai
Bodi ya Chai Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutumia teknolojia kuboresha huduma zake. “Tumeanzisha mfumo wa kidijitali unaoruhusu wakulima kusajiliwa, kufuatilia uzalishaji wao na kupata taarifa kuhusu bei na masoko moja kwa moja kupitia njia za kidijitali,” anasema Bi. Beatrice.
Pia, bodi imeanza kutumia drones na GPS mapping katika kutambua maeneo ya uzalishaji na kuboresha takwimu za sekta.
“Teknolojia imetusaidia kuongeza uwazi na ufanisi. Tunaweza kufuatilia kila hatua ya uzalishaji na mauzo, jambo ambalo linasaidia kupanga mikakati kwa uhalisia zaidi,” anaeleza.
Mikakati ya Bodi ya Chai katika miaka mitano ijayo
Akizungumzia dira ya bodi kwa miaka mitano ijayo, Bi. Beatrice anasema wanapanga kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuinua sekta ya chai unaolenga kuongeza uzalishaji, thamani na ajira.
“Tumejipanga kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 22,000 hadi kufikia zaidi ya tani 60,000 kwa mwaka. Lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa chai barani Afrika,” anasema.
Anasema wanataka kila mkoa unaolima chai uwe na kiwanda chake, jambo ambalo litapunguza gharama za usafiri na kuongeza thamani kwa wakulima. Pia wakulima wadogo watapewa nafasi ya kumiliki viwanda vidogo vya usindikaji kupitia ushirika. Hii ni hatua ya kuongeza kipato chao na kuwapa umiliki zaidi wa mnyororo wa thamani.
Sekta ya chai Tanzania inakua kwa kasi, ikichochewa na sera thabiti za Serikali, ubunifu wa Bodi ya Chai na juhudi za wakulima. Kupitia uwekezaji katika teknolojia, masoko, na usindikaji, sekta hii ina nafasi kubwa ya kuwa injini ya maendeleo vijijini.