UNICEF kwa mara nyingine tena imetahadharisha kuhusu kuzidi kuwa mbaya mgogoro wa kibinadamu huko Gaza na kusema kuwa zaidi ya watoto milioni moja katika ukanda huo bado wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji na chakula, na kuwa wengi hulala njaa kila usiku licha ya kusitishwa mapigano.
Tess Ingram, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, amesema kuwa licha ya kwamba usitishaji vita ni habari njema, lakini haitoshi kumaliza njaa na kuhakikisha kuwa familia za Gaza zinapata maji safi ya kunywa. Amesema, miundombinu ya usambazaji maji na huduma za afya huko Gaza zimeharibiwa vibaya kiasi kwamba familia zinatatizika kila siku kuishi katika mazingira hayo. UNICEF imesema licha ya kuwa misaada inayoingia Gaza imeongezeka kidogo tangu kuanza usitishaji vita, lakini bado iko chini ya viwango vya kabla ya vita na haikidhi mahitaji makubwa ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, uhaba mkubwa wa madaktari, dawa na vifaa vya tiba umepelekea maelfu ya watoto wanaohitaji matibabu kuteseka bila matibabu ya kutosha katika hospitali za Gaza. Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumzia hali ya maafa, ameeleza kuwa hali ya Gaza ni mbaya kiasi kwamba maisha ya kawaida hayawezekani kwa familia nyingi. Ugavi wa chakula na maji ya kunywa ni mdogo, watu wengi wanaishi katika maeneo ya wazi au katika makazi ya muda na hospitali zinakosa vifaa muhimu.
Kinachoendelea Gaza leo si tu janga la kibinadamu bali ni mfano wa wazi wa kushindwa kimaadili na kisiasa jamii ya kimataifa katika kutekeleza majukumu yake. Ingawa usitishaji mapigano umepunguza ghasia za moja kwa moja, lakini uharibifu mkubwa wa miundombinu na kuendelea vikwazo dhidi ya kuingizwa Gaza misaada ya kibinadamu kumezuia watu kunufaika na matokeo ya usitishaji mapigano.
Maji yasipotiririka kwenye mabomba, umeme kukatwa, viwanda vya kuoka mikate kutofanya kazi na hospitali kukosa dawa na mafuta, “usitishaji mapigano” hupoteza maana yake ya kiutendaji na kuwa kimya kinachofunika magofu tu.
Mgogoro wa sasa si matokeo ya wiki au miezi michache ya mapigano bali ni muendelezo wa miaka mingi ya mzingiro wa pande zote, uharibifu uliopangwa wa miundombinu muhimu na mashinikizo ya kiuchumi na kijamii kwa Wapalestina wanaoishi Gaza. Siasa za vikwazo vikali dhidi ya uagizaji wa mafuta, dawa, chakula, vifaa vya maji na maji taka na hata vifaa vya ujenzi zimeinyima Gaza uwezo wa kujikarabati na hata kutoa viwango vya chini kabisa vya suhula za kuendeshea maisha. Viwanda vingi vimefungwa, kilimo kimeharibiwa kutokana na ukosefu wa maji na uharibifu wa ardhi, ambapo ukosefu wa ajira umefikia kiwango cha juu kabisa.
Kutokana na hali hiyo, watu wanategemea misaada ya kimataifa kwa ajili ya mahitaji ya msingi, misaada ambayo yenyewe inakabiliwa na vikwazo na udhibiti mkali.

Mzunguko huu wenye kasoro nyingi za kiuchumi sio tu unafanya iwe vigumu kuishi, lakini pia unatishia misingi ya kijamii ya Gaza. Kizazi kipya cha watoto wa Kipalestina ambao leo wanakua kwa utapiamlo na kiu, kesho watakabiliwa na matatizo makubwa ya kimwili na kiakili. Uharibifu wa shule na vituo vya elimu unamaanisha uharibifu wa siku zijazo ambazo haziwezi kufidiwa kabisa. Maelfu ya wanafunzi wanasomea kwenye mahema na makazi ya muda, ambapo walimu walioathirika na vita pia wanajaribu kubakisha hai elimu, lakini ni wazi kuwa mfumo mzuri wa elimu hauwezi kudhaminiwa bila kuwepo usalama, lishe bora na afya endelevu. Watoto wanapolazimika kusimama kwenye foleni za kutafuta maji na chakula badala ya kuwa darasani, ina maana kwamba mustakabali wa Gaza unalengwa.
Katika mwelekeo wa kisiasa, Israel, kwa kutegemea uungaji mkono wa kisiasa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, kiuhalisia haiwajibiki mbele ya mamlaka yoyote ya kimataifa na ndio maana inaendeleza vikwazo dhidi ya wakazi wa Gaza bila kujali lolote, hata kama hilo litamaanisha kukiuka mara kwa mara masharti ya usitishaji vita uliokubaliwa na pande husika. Suala hilo kwa mara nyingine tena linaanika wazi uongo wa madai ya nchi za Magharibi kuhusu kuheshimu kwao uhuru, haki za binadamu na uadilifu. Kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya silaha ya njaa inyotumiwa na utawala wa Israel mbele ya watoto, uharibifu wa hospitali na kuzuia kuingia kwa dawa na chakula huko Gaza kumeongeza majeraha kwa watu wa Gaza.
Pamoja na hayo, lakini mapambano ya watu wa Gaza dhidi ya ukanadamizaji huo bado yanaendelea. Mashirika ya kieneo yanaendelea kusambaza chakula kwa familia zilizoathirika, makundi ya kujitolea yanahudumia watoto na walimu wanaendesha mafunzo madogo katika makazi ya wakimbizi.
Juhudi hizi zinaonyesha kuwa jamii ya Gaza bado haijakata tamaa licha ya changamoto na mashinikizo hayo makubwa yasiyo na kifani. Pamoja na hayo lakini uvumilivu huu wa kupigiwa mfano wa watu wa Gaza, sio mbadala wa wajibu wa jamii ya kimataifa.
Kile Gaza inachokihitajia sio tu malori machache ya misaada bali ni kukomeshwa mzingiro na kuanza ukarabati wa kweli. Kurejeshwa miundombinu ya maji na umeme, kuwezeshwa mtiririko wa uchumi, kurudisha hospitali na shule kwenye mzunguko wa huduma na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali muhimu za watu ndiyo misingi ya maisha. Ikiwa kweli ulimwengu unadai kutetea haki za watoto, ni lazima utumie njia za kisiasa, kisheria na kiuchumi kuulazimisha utawala wa Kizayuni ufuate misingi ya sheria za kimataifa. Wataalamu wanasisitiza kuwa bila kuondolewa mzingiro na kuanza ujenzi mpya wa kimuundo, Gaza itasalia katika mzunguko wake wa kudumu wa mgogoro wa hivi sasa.
Mustakbali wa Gaza bado unaweza kuandikwa, lakini si kwa lugha ya mzingiro na uharibifu, bali kwa uadilifu, wajibu na ubinadamu. Siku ambayo watoto wa Gaza hawatakuwa na njaa na kulala kwa amani, kwenda shule na kuwaza juu ya mustakabali mzuri zaidi kuliko siku za nyuma, hiyo ndiyo siku ambayo ulimwengu utaweza kudai kwamba haujakaa kimya mbele ya maafa haya ya kutisha.