
Kenya imeitaka Tanzania itoe majibu kuhusu hali ya raia wake waliojipata kwenye mzozo wa baada ya uchaguzi, huku ikishinikiza serikali ya nchi hiyo ihakikishe usalama wao na kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa haki zao.
Hayo yanajiri baada ya taarifa kuongezeka kuwa Wakenya walioko Tanzania wanaishi kwa hofu na vitisho vya kunyanyaswa wakishukiwa kushiriki maandamano yaliyosababishwa na uchaguzi wa Oktoba 29 na matokeo yake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, katika siku za hivi karibuni, familia za Wakenya zimeeleza hofu zao kuhusu usalama wa wapendwa wao walioko Tanzania, huku ripoti zikionyesha baadhi ya raia hao wameuawa, wengine wakikosa kufahamika waliko au wakiwa hospitalini, na wengine wakizuiliwa na polisi.
Familia ya mmoja wa Wakenya ilitangaza siku ya Jumanne kuwa walikuwa na taarifa za kuaminika kuwa mwana wao, mwalimu aliyefanya kazi Dar es Salaam, aliuawa, lakini hawakuweza kupata mwili wake.
Jana Alkhamisi, Novemba 6, Mkuu wa Mawaziri wa Kenya na Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo walifanya kikao ambapo Kenya ilisisitizia hakikisho la usalama wa raia wake.
“Wakati wa mazungumzo, tulisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa raia wote wa kigeni, wakiwemo Wakenya, ambao wanachangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia biashara halali na huduma za kitaalamu,” alisema Mudavadi baada ya mazungumzo hayo huku akithibitisha ripoti za kutokea mauaji, kuzuiliwa na kunyanyaswa Wakenya na maafisa wa Tanzania.
Aliongezea kwa kusema: “kuna matukio yaliyoripotiwa ambapo haki za Wakenya wengi zimekandamizwa, na kesi hizi zimefikishwa rasmi kwa serikali ya Tanzania”…/