Maandamano hayo ya vijana yalikuwa yanapinga uchaguzi huo wa Oktoba 29. Chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, na baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanasema maafisa wa polisi waliwaua zaidi ya watu 1,000.
Serikali imesema idadi hiyo imetiwa chumvi lakini yenyewe hadi sasa haijatoa takwimu za vifo vilivyotokea.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, polisi ya nchi hiyo ilitoa tangazo yenye orodha ya majina 10 ya watu inawasaka katika uchunguzi wake wa machafuko yaliyojitokeza.
Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya waendesha mashtaka kuwapandisha kizimbani karibu watu 200 kwa makosa ya uhaini.
Haya ni mashtaka ya kwanza dhidi ya watu wanaoshukiwa kushiriki maandamano.
Hati ya mashtaka dhidi ya washtakiwa zaidi ya 90 iliyowasilishwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Dar es Salaam imesema washtakiwa “walibuni njia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 kwa madhumuni ya kuitisha ofisi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” na kusababisha uharibifu wa mali za umma.
Hata hivyo hakukuwa na ufafanuzi zaidi kuhusu mashtaka hasa dhidi yao, isipokuwa dhidi ya mshtakiwa mmoja, ambaye ni mfanyabiashara Jenifer Jovin Bilikwija, maarufu Niffer.
Niffer ameshitakiwa kwa kosa la uhaini, akidaiwa kuwahamasiha wananchi kuvuruga uchaguzi na kuwahimiza kununua barakoa za kujizuia na gesi ya kutoa machozi wakati wa maandamano, dukani kwake.
Makosa ya uhaini nchini Tanzania, mara nyingi huchukuliwa kuwa nyeti kisiasa na adhabu yake huwa ni kunyongwa hadi kufa.
Viongozi wa upinzani wanaosakwa na polisi
Miongoni mwa wanaotafuta ni katibu mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, naibu wake Amaan Golugwa na msemaji wa chama hicho Brenda Rupia. Taarifa za mapema Jumamosi zilisema Golugwa alikuwa tayari amekamatwa jijini Dar es Salaam.
“Jeshi la polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, linaendelea kuwasaka wote waliopanga, kuratibu na kutekeleza uovu huo,” imesema sehemu ya taarifa iliyotolewa na polisi.
Juhudi za kuwapata viongozi hao na chama chao kutoa tamko kuhusu msako wa polisi hazikuzaa matunda. Kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, hivi sasa yuko korokoroni akikabiliwa na kesi ya uhaini.
na kushindwa kwake kushiriki uchaguzi mkuu pamoja na mgombea mwingine chama cha upinzani, ndio inaaminika kuwa chanzo cha maandamano ya umma.
Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa asilimia 98 ya kura. Kiongozi huyo aliapishwa siku ya Jumatatu kuendelea kuitawala nchi hiyo.
Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika wamesema kura hiyo haikuwa ya kuaminika na kwamba walishuhudia masanduku yaliyotiwa kura zisizo halali. Serikali imepuuzilia mbali ukosoaji huo na kuwa uchaguzi wa usawa.
Maandamano ya umma yalizuka mnamo Oktoba 29 kwenye miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya pamoja na mikoa mengine kote nchini humo. Hayo yamesemwa katika taarifa ya polisi, tamko ambalo limetoa kwa mara ya kwnaza picha pana ya ukubwa wa ghasia hizo zilizoshuhudiwa nchini humo.
Polisi imesema watu walijeruhiwa bila kutoa maelezo zaidi, huku mali za umma na binafsi ikiwemo mashine za kutoa pesa na ofisi za serikali viliharibiwa.
Makundi ya kiraia yasema kulikuwa na “mauaji ya kulipa kisasi”
Hapo jana Ijumaa, makundi ya haki za binaadamu nchini Tanzania yalilaani ripoti za kile walichotaja “mauaji ya kulipiza kisasi” dhidi ya raia, katika ghasia hizo za baada ya uchaguzi.
Katika taarifa ya pamoja na mashirika mengine sita yasiyo ya kiserikali, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilisema kulikuwa na “matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao hawakuwa na silaha, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kulipiza kisasi dhidi ya raia, baadhi wakiwa majumbani mwao.”
Taarifa hiyo imesema, “Familia zimeachwa zikiwa na kiwewe, na watoto wameshuhudia wazazi wao wakidhulumiwa.”
Imeongeza kuwa mamia ya watu walikamatwa, na baadhi wameendelea kuzuiliwa bila dhamana.
Taarifa hiyo ilionya kwamba “kiwango cha ukiukwaji wa haki za binadamu bado hakijawekwa wazi kikamilifu”, huku ikikosoa hatua ya kufungwa kwa intaneti na mipaka kwa vyombo vya habari.
