Kauli ya Waziri Kombo inakuja wakati Umoja wa Ulaya ukiwa umepanga kuipa Tanzania zaidi ya uero milioni 150 sawa na Tsh 400 bilioni, fedha za miradi ya maendeleo kwa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2026.
Akizungumza na wanahabari, leo Waziri huyo mwenye dhamana ya ushirikiano wa kimataifa, amesema, watanzania hawatakufa kwa njaa kwa kukosa fedha hizo.
“Kwa Hiyo balozi wetu aliandika barua kwa bunge la ulaya kwa ajili ya kupata maelezo, barua ile ikarushwa na wao wenyewe kutokana na ushabiki mbalimbali, kwa barua ile hatujaathirika kwa sababu barua ile imekwenda kisheria na haki”, alisema Kombo.
Hata hivyo Waziri Kombo amesema serikali inafuatilia kwa karibu suala hilo kupitia kwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji yalipo makao makuu ya umoja huo, Jestas Nyamanga, na hivyo serikali itatoa kauli rasmi baada ya kupokea taarifa kamili ya mjadala huo kutoka kwa Balozi wake kwenye Umoja wa Ulaya.
Jumatano, Bunge la EU, katika kikao chake lilijadili vurugu za maandamano yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania Oktoba 29, na kuadhimia kusitisha msaada wa kifedha uliopangwa kutolewa kwa taifa hilo la Afrika mashariki.
“Umoja wa ulaya unatakiwa kusimamisha misaada yake ya kifedha kwa Tanzania, uhusiano huo unatakiwa kuundwa kwa kuendana na utawala bora, uhuru kamili na uwajibikaji”, ilielezea taarifa ya bunge hilo.
“Kauli hiyo sio ya kidiplomasia”
Hata hivyo bado azimio hilo litahitaji baraka za baraza la Umoja wa Ulaya na tume ya Umoja huo, kabla ya kutekelezwa kwake.
Wachambuzi wa masuala ya diplomasia Tanzania wamesema kauli ya Waziri Kombo, inahitaji kuchakatwa ingawa kama taifa ni sahihi kuanza kutegemea rasilimali zake. Mhadhiri wa Shule ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema kauli ya Waziri Kombo sio ya Kidiplomasia.
“Kauli hiyo sio ya Kidiplomasia kwa sababu nchi zilizoenelea kama za Ulaya hazisaidii nchi zianzoendelea kwa maana ya kutoa misaada tu, nchi zilizoendelea zinahitaji vile vile mikopo ya masharti nafuu nchi hizo zinahitaji hadi mikopo ya bei nafuu kwa benki kubwa, ambazo wahisani wakubwa wa benki hizo au wenye hisa wakubwa wa benki hizo ni nchi hizo hizo za magharibi”, alisema Mbunda.
Azimio hilo limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu mauaji ya raia, utekaji wa wanaharakati na ukandamizaji wa wafuasi wa upinzani, huku likitaja kesi ya Uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu kuwa imechochewa kisiasa.