Dar es Salaam. Wakati jitihada za kuendelea kuvutia wawekezaji zikipamba moto nchini, Serikali imewaita Watanzania wanaotaka kujenga viwanda kuchangamkia fursa ya kupewa ardhi bure iliyotolewa na Serikali.

Ardhi hiyo inatolewa kupitia maeneo maalumu ya kiuchumi yaliyotengwa kote nchini ikiwa ni moja ya hatua ya kuendelea kuwavuta Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini hususan kwenye uongezaji wa thamani.

Hayo yamesemwa leo Desemba Mosi, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri wakati akizungumza kwenye mkutano wa wafanyabiashara ulioandaliwa na Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Utoaji ardhi unawekwa wazi wakati ambao EABC na TCCIA wameanika mkakati wa kuwainua vijana ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika ufanyaji wa biashara zao na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza Teri amesema mpango wa utoaji ardhi ya bure kwa Watanzania wanaotaka kujenga viwanda kwa mara ya kwanza ulitangazwa Julai 16 mwaka huu na tayari walioomba na kupitishwa baada ya kukidhi vigezo.

“Kuna maombi ya watu tunayapitia, wiki hii kuna watano watakabidhiwa maeneo ili waweze kuanza kazi. Moja ya sharti ni kuhakikisha ujenzi unaanza ndani ya miezi 12 tangu unapopewa eneo,” amesema.

Amesema kupitia utaratibu huo ambao Mtanzania halipii hata shilingi moja,  humuwezesha kupewa hati ya umiliki wa hadi miaka 33 kabla ya ardhi kurudishwa serikalini.

Teri ameitaja hiyo kuwa fursa ya Watanzania kuwa na ubia na wazalishaji wa nje kwani inaruhusiwa Mtanzania kutumia mtaji wa mwekezaji kutoka nchi yoyote ili kufanikisha azma hiyo.

“Kama una mtu huwa unachukua mizigo kutoka kwake kama yuko China ni wakati wako wa kumshawishi aje awekeze Tanzania, mnaingia naye ubia wewe unapata ardhi bure katika maeneo yaliyopangwa, ila kwa sharti moja ni lazima akupe umiliki wa asilimia 30,” amesema Teri.

Amesema mbali na kupewa ardhi bure sheria imewapa nafuu nyingi wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani ikiwemo msamaha wa kodi katika baadhi ya huduma wanazozitoa kulingana na sekta husika.

Teri amesema yapo maeneo mengi yaliyotengwa ikiwemo Bunda, Tanga, Kwala, Bagamoyo, Songea yakiwa na huduma zote muhimu za kijamii ikiwemo maji, umeme na miundombinu ya kusafirisha bidhaa.

“Ukija kwetu kutaka ardhi hii, ndani ya siku saba tutakuwa tumekupa mkataba wa kuanza ujenzi baada ya kujiridhisha,” amesema.

Hilo linaenda sambamba na Tiseza kutafuta Mtanzania au kampuni inayoweza kusaidia wengine kuuza bidhaa zao nje ya nchi ili aweze kupewa ofisi kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kuuza bidhaa kirahisi.

Hili linafanyika wakati ambao Tiseza imepewa lengo la kusajili miradi 1,500 katika mwaka wa fedha 2025/2026 yenye thamani ya zaidi ya Sh35.67 trilioni.

Ili kufanikisha hilo iliwekwa mikakati maalumu nane ambapo miongoni mwake ni kuwezesha vijana kushiriki katika uwekezaji kupitia uanzishwaji wa ofisi maalumu itakayowasaidia kufanya uwekezaji sambamba na kutengewa maeneo maalumu ya uwekezaji kwenye mikoa tofauti nchini.

Hiyo inalenga kuwafanya kushiriki katika ujenzi wa uchumi shirikishi sambamba na kutengeneza fursa za ajira kwao, kujiajiri na kiweza kuajiri wengine ili kupunguza wimbi la wahitimu wasio na ajira.

Akielezea namna TCCIA inavyosaidia wawekezaji kupata ardhi hiyo, Rais wa Chemba, Vincent Minja wameongeza nguvu katika kuvutia wawekezaji wa ndani ili Watanzania wawe sehemu ya uchumi ili kuongeza ajira na vijana watakuwa na nguvu ya kushindana na wengine.

Amesema kama TCCIA wamekuwa wakiwapokea wawekezaji wote wanaopitia kwao kabla ya kwenda Tiseza huku viwanda ikiwa ni sekta iliyowekewa mkazo.

“Tunahitaji teknolojia na ili tuipate lazima tupate watu wenye fedha na wawekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, mtu anakuja na teknolojia yake na watu wachache ambao watafundisha watu wetu,” amesema Minja.

Akielezea walivyopanga kuwasaidia vijana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa EABC, Imani Majula amesema wamekuwa wakitafsiri fursa na kuzitumia kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kupitia makubaliano na TCCIA waliweka azma ya kuandaa majukwaa ambayo yanaweza kutumika kutafsiri fursa ambazo watanzania wanaweza kuzipata nchini kwao.

Ili kufanikisha hilo wamekuwa wakikuza uwezo wa Watanzania ikiwemo vijana na kanzidata waliyoanzisha wamelenga kutambua sehemu walipo, mahitaji yao na wanawezaje kusaidiwa.

“Hiyo kanzidata ni muhimu na tunaitekeleza kwa kushirikiana na TCCIA kwenye wilaya 101 na mikoa 26. Hivyo mkutano kama huu utafanyika tena Arusha kwa wiki mbili zijazo, Mwanza pia tutaifanya,” amesema Majula.

Amesema hilo litaanza kupitia utambuzi huku eneo ambalo litaangaliwa sana ni upatikanaji wa mitaji wakati ambao wakopeshaji wanataka anayepewa fedha awe na elimu nayo pamoja na suala la uwekaji wa akiba.

“Pia, kujua fursa zilizopo. Hata ukitaka kufanya biashara ni lazima ujue fursa ni zipi, eneo tulilogundua kwa vijana ni uwezo wa kuongeza thamani kwa mfano yule aliye Tukuyu wanalipa parachichi ambalo linaweza kuzalisha shampoo, dawa hivyo tutajikita huko kwenye kuongeza thamani,” amesema.

 Amesema utoaji wa ujuzi huo utafanyika kupitia vituo atamizi vitakavyokuwa katika kila wilaya ndani ya ofisi za Tiseza ili kuhakikisha kila kijana anafikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *