
Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na Simba Developers Limited imesaini makubaliano ya kimkakati yanayolenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora na nafuu kwa Watanzania, kupitia mpango maalumu wa mikopo ya nyumba.
Kupitia ushirikiano huo, wateja watakaonunua nyumba za kisasa zinazojengwa na Simba Developers watapata mikopo yenye masharti nafuu kupitia bidhaa ya Exim Bank ijulikanayo kama ‘Nyumba Yangu’.
Mpango huu unatokana na ongezeko la mahitaji ya makazi ya bei nafuu katika miji na maeneo ya pembezoni, ambako wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya gharama kubwa na ugumu wa kupata mikopo rafiki.
Kwa mujibu wa Benki ya Exim, wateja sasa wanaweza kukopa hadi Sh1 bilioni kwa wateja wa Personal na Preferred Banking, na hadi Sh1.5 bilioni kwa wateja wa Elite Banking, wote wakiwa na masharti nafuu ya riba.
Akizungumza wakati wa utiliaji saini, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lymo, alisema hatua hiyo inalenga kusaidia Watanzania wengi kufanikisha ndoto zao za umiliki wa makazi.
“Kumiliki nyumba ni moja ya mafanikio makubwa kwa Watanzania wengi. Kupitia ushirikiano huu na Simba Developers tunarahisisha safari ya ununuzi wa nyumba kwa kutoa mkopo kulingana na uwezo wa mteja, hivyo kuwawezesha watu wengi zaidi kupata makazi yao ya kudumu,” alisema Lymo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Simba Developers, Yusuf Hatimali Ezzi, alisema kampuni yake inajikita katika ujenzi wa nyumba za kisasa zenye ubora wa kimataifa, na ushirikiano na Benki ya Exim utaongeza kasi ya upatikanaji wa makazi hayo kwa wananchi.
“Nyumba zetu zimejengwa kwa viwango vya juu, zikiwa salama na za kisasa. Ushirikiano huu unatoa fursa kwa wanunuzi kupata fedha kwa haraka na kwa urahisi, na hivyo kuwezesha familia nyingi kufikia ndoto ya kuishi kwenye makazi bora,” alisema Ezzi.
Makubaliano hayo yanaiweka Exim Bank katika nafasi nzuri zaidi kwenye soko la mikopo ya makazi, kipindi ambacho mahitaji ya huduma za kifedha kwa ajili ya ununuzi wa nyumba yanaendelea kuongezeka nchini.
Kupitia mpango huu, upatikanaji wa makazi bora na ya kisasa utaongezeka kwa kiwango kikubwa, huku Benki ya Exim ikithibitisha dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya taifa kupitia upanuzi wa mikopo ya makazi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Kwa wateja, mpango huu unarahisisha kupata mikopo, unatoa chaguo mbalimbali za kifedha na kuwawezesha kufanya maamuzi ya umiliki wa nyumba kwa kujiamini hatua itakayoboresha usalama wao wa kifedha pamoja na ustawi wa familia zao.