
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Neo Maema, amesema kitendo cha timu hiyo kupoteza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, hakuna wa kulaumiwa zaidi ya wachezaji wenyewe.
Maema ameyasema hayo muda mfupi baada ya Simba kufungwa mabao 2-1 na Stade Malien katika mechi ya pili Kundi D la michuano hiyo iliyochezwa jana Jumapili Novemba 30, 2025 nchini Mali.
Kabla ya mechi hiyo, Simba ilipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico na kuwafanya wawakilishi hao wa Tanzania kuburuza mkia wa Kundi D ikiwa haina pointi.
Maema ambaye alifunga bao pekee katika kichapo hicho cha jana, amesema: “Kiukweli inavunja moyo. Tumejiangusha wenyewe na mashabiki ambao wamekuwa wakituunga mkono. Hata benchi la ufundi limekuwa likitusukuma sana.
“Inauma kupoteza mechi mbili mfululizo kwa timu kubwa kama Simba. Nadhani tunapaswa kuchambua mchezo kama wachezaji kila mmoja kwa nafasi yake na kurudi kupigania nembo ya klabu. Hii ni klabu kubwa, hatuna cha kujitetea, tucheze nyumbani au ugenini, tunapaswa kufanya bora zaidi.”
Simba katika mechi hiyo iliruhusu mabao mawili kipindi cha kwanza yaliyofungwa dakika ya 16 na 23 kupitia Taddeus Nkeng Fomakwang na Ismaila Simpara.
Mabao hayo kwa kiasi fulani yamemuumiza Maema aliyetua Simba msimu huu akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini akisema: “Inaumiza kuruhusu magoli mawili kipindi cha kwanza. Ni makosa yetu.
“Lakini kitu chanya tunachoweza kuchukua ni kwamba wachezaji sasa tunaweza kuona kiwango cha Ligi ya Mabingwa hakuna timu ndogo, kila timu inashindana.
“Nadhani tunapaswa kurudi upya. Inaumiza. Inahuzunisha. Sio vizuri. Nafikiri tutakaporudi kuendelea mwaka ujao tutakikisha tunapata alama nyingi.”
Simba imebakiza mechi nne katika Kundi D ambazo inatakiwa kutoangusha pointi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali.
Kati ya Januari 23 na 25, 2025, Simba itakuwa Tunisia kukabiliana na Esperance, kisha zitarudiana jijini Dar kati ya Januari 30 na Februari 1, 2026.
Simba itaifuata Petro Atletico nchini Angola, mechi ikichezwa kati ya Februari 6 na 8, 2026, kisha itamalizia hatua ya makundi nyumbani dhidi ya Stade Malien kati ya Februari 13 na 15, 2026.