Dar es Salaam. Wahitimu wamehimizwa kuendelea kulinda na kudumisha amani, mshikamano na umoja katika jamii sanjari na kutambua mchango wao kama vijana wanaojitambua katika kuendeleza Taifa.

Wito huo umetolewa leo Desemba 1,2025 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye katika duru ya nne ya mahafali ya 55 ya chuo hicho.

Anangisye amesema uhai, usalama, maendeleo na ustawi wa Taifa lolote duniani unawategemea vijana. “Hakuna mtu asiyejua mchango wa vijana katika Taifa hivyo tumieni ujana wenu kwa faida, popote mlipo au mtakapokuwa msichoke kulinda amani.”

Amewasisitiza kuwa thamani ya elimu waliyoipata wakahakikishe inaonekana katika jamii kwa kuitumikia kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo.

“Katika maisha yenu ya kila siku mzingatie maadili ya jamii ya Tanzania na Afrika kwa ujumla ya ughaibuni waachieni ughaibuni,” amesema.

Amewasihi kuwa wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika pale inapotokea ajira za Serikali au sekta binafsi zitakapochelewa kupatikana.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete amesema anafurahishwa kuona ongezeko la idadi ya wahitimu katika ngazi za uzamivu, huku akiwahimiza kutumia elimu yao katika kuleta mapinduzi kwenye sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Katika mahafali hayo ya 55 duru ya nne jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa shahada ya uzamivu kati yao 45 ni wanaume na 20 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 30.8

Naye Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Balozi Mwanaidi Maajar amewasisitizia kwenda kudhihirisha taaluma zao kwa vitendo kwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Amesema baraza linaendelea kuwasisitiza wazazi na walezi kusimamia misingi bora ya malezi kwa watoto haswa katika kipindi hiki cha utandawazi, kwani bila kufanya hivyo kutakuwa na kizazi tegemezi ambacho hakiwezi kuwajibika ipasavyo.

Katika duru ya nne ya mahafali ya 55 ya UDSM jumla ya wahitimu 2,046 walitunukiwa.

Wahitimu wa shahada ya uzamivu ni 65, umahiri 522, stashahada ya uzamili 26, shahada ya awali 1,291, stashahada 126 na astashahada 16.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *