Mwanza. Zaidi ya watu 560 waliokuwa wakitapika damu kutokana na ugonjwa wa kichocho cha tumbo wamefanyiwa matibabu kwa kutumia mashine ya picha ya ndani ya utumbo (endoscopy) katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza. Watu hao ni kati ya 666 waliofanyiwa uchunguzi.

Watu hao walipata matibabu hayo kuanzia mwaka 2023 hadi sasa, baada ya utafiti kubaini idadi kubwa ya wagonjwa kutapika damu wakati wa utekelezaji wa Mradi wa kudhibiti kichocho katika Wilaya ya Ukerewe (2021/25).

Akitoa taarifa ya ugonjwa wa kichocho katika vijiji 35 vilivyofikiwa na mradi huo leo Jumatatu Desemba Mosi, 2025 katika hafla fupi ya kukabidhi mashine nyingine ya endoscopy, Mratibu wa mradi huo, Dk Stella Mugassa, amesema changamoto ya kutapika damu hasa kwa wanaume wenye kichocho ilikuwa kubwa.

Amesema wakati mradi unaanza mwaka 2021 walifanya uchunguzi wa maambukizi ya kichocho katika vijiji 20 vya awali kwa kuchukua sampuli ya watu takribani 200 kila kijiji, ambapo matokeo yalionesha kati ya watu 10 watano walikuwa na kichocho.

Ameeleza kuwa changamoto nyingine kubwa waliyokutana nayo ni tatizo la wagonjwa kutapika damu, ambapo katika wodi kulikuwa na wagonjwa wengi wenye dalili hiyo.

“Kutapika damu inatokana na vitu tofautitofauti lakini kwa sababu tulikuwa tunashughulika na vichocho ndio hapo endoscopy ilipoingia…katika kufahamu watu wangapi wanatapika damu na kwa sababu gani?

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mashine ya endoscopy iliyofanyika katika hospitali ya wilaya hiyo.

“Kwa kutumia endoscopy tuligundua kuwa asilimia 48 ya wagonjwa waliokuwa wakitapika damu ilitokana na matatizo ya ini na bandama, lakini baada ya matibabu kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 15,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mugassa, kundi lililoathirika zaidi lilikuwa la watu wenye umri kati ya miaka 30 hadi 69, hususani wanaume wanaojishughulisha na uvuvi ambao hukaa muda mrefu majini na kuwa katika hatari ya maambukizi.

“Katika vijiji 20 vilivyoanza kufanyiwa utafiti mwaka 2021, kiwango cha maambukizi kilifika hadi asilimia 45, sawa na watu watano kati ya 10 kuwa na kichocho.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), jamii ikifika kiwango cha maambukizi cha asilimia 10 inapaswa kupatiwa dawa ya kinga, hali iliyofanya vijiji vyote vilivyohusika kuanza kupewa matibabu,”amesema.

Akizungumzia athari za ugonjwa huo, amesema husababisha tumbo kujaa maji, kuvimba kwa ini na bandama pamoja na kutokwa damu kupitia njia ya haja kubwa.

Mtafiti wa ugonjwa wa kichocho kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Kikatoliki (CUHAS), Profesa Humphrey Mazigo, amesema kupitia mradi huo, vijiji 35 kati ya 79 vya wilaya hiyo vimenufaika na kampeni za kinga tiba kwa zaidi ya miaka mitano, ambapo zaidi ya watu 300,000 wamepatiwa dawa ya praziquantel na maambukizi yamepungua kwa takribani asilimia 70.

Amesisitiza kuwa ili kudhibiti kabisa ugonjwa wa kichocho, ni muhimu kuimarisha upatikanaji wa maji safi na matumizi sahihi ya vyoo, hasa katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Victoria.

Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Dk Charles Mkombe amesema hapo awali wodi ya wanaume ilikuwa inajaa wagonjwa waliokuwa wakitapika damu, lakini sasa hali imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na upatikanaji wa huduma hizo.

“Matibabu yote yanatolewa bila malipo na sasa unaweza kukaa hata wiki bila kupata mgonjwa wa kutapika damu,” amesema.

Naye, Mkuu wa Chuo cha CUHAS, Profesa Erasmus Kamugisha amesema katika mradi huo unaofadhiliwa na Else-Kroner Fresenius chini ya Else Kroner Centres na kutekelezwa na chuo hicho, ulidhamini masomo ya shahada ya uzamili katika eneo la magonjwa ya ndani kwa daktari mmoja na kuwadhamini madaktari wawili na wauguzi wawili waliopata mafunzo katika kitengo cha endoscopy, ili kukisimamia na kutoa huduma bora za kibingwa.

Amesema ujenzi na uimarishwaji hospitali za ngazi za chini hasa kupitia ujuzi, vifaa na mashine za endoscopy ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa kubaini na kutibu wagonjwa wa kichocho na kupunguza madhara, vifo na gharama za matibabu.

Akipokea mashine ya endoscopy, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai ameishukuru CUHAS na Hospitali ya Bugando kwa kushirikiana katika kutoa huduma hiyo kwa wakazi wa Ukerewe.

“Mradi huu umetusaidia si tu kwa kuleta mashine ya endoscopy, bali pia kwa kuokoa maisha ya wananchi wetu ambao wangelazimika kutumia gharama kubwa kusaka huduma hizo nje ya eneo letu,” amesema.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha takribani Watanzania milioni 22 sawa na asilimia 52 hupata maambukizi ya ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo kila mwaka, huku Kanda ya Ziwa ikiongoza kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 50 hadi 80.

Tatizo la ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo mkoani Mwanza linasababishwa na jiografia yake ya kuwa na maji mengi, shughuli za kilimo (majaruba ya mpunga) asili ya madimbwi ya maji na hivyo wananchi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo.

Dalili za awali za kichocho huanza kuonekana wiki chache baada ya mtu kuingia kwenye maji yaliyoathiriwa na minyoo aina ya schistosoma, lakini mara nyingi hupuuzwa kwa kudhani ni homa ya kawaida.

Mratibu wa mradi wa kichocho wilayani Ukerewe, Dk Stella Mugassa akielezea ugonjwa wa kichocho katika wilaya hiyo.

Wagonjwa huanza na homa, ganzi za mwili, kikohozi na muwasho kwenye ngozi. Hizi ni dalili ambazo watu wengi huzipita bila kuelewa kuwa tayari wameambukizwa kichocho.

Hata hivyo, dalili hutofautiana kulingana na aina ya kichocho. Aina inayoshambulia kibofu cha mkojo, ambayo ni ya kawaida zaidi Tanzania, hujionyesha kwa mkojo wenye damu, maumivu ya chini ya tumbo na kukojoa mara kwa mara.

Kwa upande wa kichocho cha utumbo, mgonjwa hupata kuhara chenye damu, maumivu makali ya tumbo, gesi nyingi na kupungua uzito.

Wataalamu wanabainisha kuwa athari za muda mrefu ni kubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na matatizo ya figo, ini, na mishipa ya damu, pamoja na uvimbe wa tumbo kutokana na kuongezeka kwa maji (ascites).

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa wananchi kuepuka kuoga, kuogelea au kuchota maji kwenye mabwawa na mito isiyo salama, pamoja na kutafuta matibabu mapema wanapoona dalili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *