Afisa wa zamani wa jeshi la Uingereza amefichua mauaji yaliyofanywa na askari wa kikosi maalumu cha Uingereza nchini Afghanistan na jinsi makamanda wa kikosi hicho walivyonyamazia kimya na kuficha uhalifu huu.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa zamani katika jeshi la Uingereza amefichua uhalifu huo wakati wa uchunguzi wa umma na kusema kwamba askari wa kikosi maalumu wa Uingereza nchini Afghanistan waliwaua washukiwa kati ya 2010 na 2013, kitendo kinachotambuliwa kama uhalifu wa kivita.

Ushahidi huu unaonyesha kwamba uongozi wa jeshi la Uingereza ulikuwa na habari kuhusu uhalifu huo lakini haukuchukua hatua yoyote.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeagiza uchunguzi ufanyike kuhusu uhalifu huo baada ya makala ya BBC kufichua kwamba watu 54 waliuawa kiholela na askari wa kikosi cha SAS.

Lengo la hatua hiyo ni kuchunguza ukweli wa mauaji hayo yaliyofanyika kinyume cha sheria, kiwango cha uzito wa uchunguzi wa awali wa polisi wa kijeshi na uwezekano wa kufichwa kesi hiyo. Jaji Charles Haddon-Keef, mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa kesi hiyo, amesisitiza haja ya kuwafikisha mahakamani wale wote waliohusika na uhalifu huo.

Kuhusu uhalifu huu wa kivita, afisa wa jeshi la Uingereza, anayetajwa kwenye vyombo vya habari kama “N.1466”, ameeleza kwamba tangu 2011 alikuwa akishuku tofauti iliyokuwepo kati ya idadi ya waliouawa na silaha zilizotwaliwa na askari wa Uingereza, na aliliona jambo hilo kama ishara ya mauaji kinyume cha sheria.

Baadaye afisa huyo alijuta kwa kutotoa taarifa mapema kwa polisi wa kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *