
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: “Baada ya raundi tano za mazungumzo, wakati Iran ilipokuwa ikijiandaa kwa raundi ya sita, Marekani ilikiuka njia ya kidiplomasia na juhudi za upatanishi.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo katika mahojiano na kipindi cha “Pamoja na Musa Al-Farai” jana Jumatatu na kuongeza kuwa: “Inasikitisha kwamba sheria na mifumo ya kimataifa imeathiriwa na mienendo ya Marekani ya kutumia mabavu katika mahusiano ya kimataifa.”
Araqchi ameongeza kuwa: “Suala hili linaonekana wazi katika uvamizi wa kiholela wa kijeshi na utekelezaji wa operesheni za kigaidi wakati wowote Marekani inapotaka.” Sayyid Araqchi amesisitiza kuwa: “Tunachoshuhudia hii leo kimesababisha wasiwasi mkubwa duniani.”
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, mlango wa mazungumzo na upatanishi uko wazi wakati wote, alimradi sheria na kanuni zifuatwe.
Amesema kushindwa kwa mazungumzo ya mwaka huu kulitokana na uchoyo na kupenda makuu kwa Marekani.
“Tatizo kuu la mazungumzo ya mwaka huu lililosababisha kushindwa kwake ni mienendo ya Marekani ya kulazimisha matakwa yake; waliingia katika mazungumzo hayo wakiwa na sera ya “kusitishwa kikamilifu” urutubishaji wa madini ya urani nchini Iran”, amesema Sayyid Araqchi na kusisitiza kuwa: Hakuna nchi inayoweza kunyimwa haki zake halali.