Dar es Salaam. Mastaa wa Bongofleva, Diamond Platnumz na Rayvanny wamerekodi pamoja nyimbo nyingi tena zilizofanya vizuri kiasi kwamba ni vigumu kuamini kama kuna wanamuziki wengine watakuja kufikia rekodi hiyo.

Tangu 2016 wameachia kolabo zaidi ya 10 ambazo hazipo katika albamu wala Extended Playlist (EP) ya pamoja. Hii ni ishara ya matokeo mazuri ya kila kazi wanayotoa na ndio sababu ya kufikia hapo.

Itakumbukwa Rayvanny alijiunga na WCB Wasafi 2015 akitokea Tip Top Connection alikokuwa tangu 2012 kupitia Babu Tale, lakini akaishia kurekodi wimbo mmoja tu (Upo Mwenyewe) ambao haukufanya vizuri.

Wimbo wake wa kwanza, Kwetu (2016) chini ya WCB Wasafi ambao pia ndio ulimtambulisha video yake ilishika namba sita kati ya 15 zilizotazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube Tanzania mwaka huo.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo, akachaguliwa kuwani tuzo za Africa Entertainment Awards, USA (AEAUSA) 2016 kama Best New Artist na Best New Talent, pia aliwania MTV MAMAs kama Best Breakthrough Act. 

Hata hivyo, baada ya takribani miaka sita ya kufanya kazi pamoja tena kwa mafanikio makubwa, hatimaye Rayvanny aliachana na lebo hiyo yake Diamond akiwa tayari amefungua yake, Next Level Music (NLM).

Ikumbukwe chini ya usimamizi wa WCB Wasafi, Rayvanny aliachia EP tatu, Flowers (2020), New Chui (2021) na Flowers II (2022), pamoja na albamu moja, Sound From Africa (2021).

Na baada ya kuondoka WCB Wasafi ametoa EP moja, Unplugged Session (2022) na albamu moja, The Big One (2024) yenye nyimbo 18, miradi yote hii ikisimamiwa na lebo yake, NLM.

Licha ya kuondoka WCB Wasafi, Rayvanny aliendelea kuwa karibu na Diamond hadi kutoa kazi nyingine pamoja ingawa wengi hawakutegemea hilo kutokana na historia ya wasanii walioondoka katika lebo hiyo.

Kazi zilizotoka baada ya kuachana na WCB Wasafi ni Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024), zote zikitayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic.

Hapo awali, wawili hao walishatoa nyimbo kama Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020) na Woza (2020), kolabo ya kwanza yenye midundo ya Amapiano.

Ikumbukwe wimbo wao, Nitongoze (2022) ulifanya vizuri hadi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana, na ulijumuishwa katika albamu, The Big One (2024).

Kati hizo 10, nyimbo nane za mwisho ni zake Rayvanny akimshirikisha Diamond, huku mbili ya mwanzo ni za Diamond akimpa shavu Rayvanny, mshindi wa tuzo ya BET 2017.

Pia usisahau mastaa hao wamekutana kwenye ngoma mbili zilizokutanisha wasanii wote wa WCB Wasafi, Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020), hivyo kufanya jumla ya nyimbo 12 walizorekodi pamoja. 

Kwa kipindi cha miaka minane iliyopita, hakuna wasanii Bongo walioshirikiana zaidi ya hawa, huku Rayvanny akiwa ndiye msanii aliyemshirikisha Diamond kwenye nyimbo zake nyingi kwa muda wote!.

Kabla ya kutoka, Rayvanny alikuwa na ushirikiano mkubwa wa kikazi na Diamond, amechangia melodi kwenye wimbo wa Diamond, Make Me Sing (2016), na Zigo Remix (2016) wake AY akishirikiana na Diamond.

Utakumbuka naye Rayvanny ameshirikiana sana na msanii aliyemtoa kimuziki chini ya NLM, Mac Voice ambaye alimtambulisha mnamo Septemba 2021 kupitia EP yake, My Voice (2021).

Wawili hao ambao kwa sasa wanaonekana kupishana kikazi, walifanikiwa kutoa kolabo tano – Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021), Muongeze (2022) na Mwambieni (2023).

Hivyo hadi sasa Rayvanny ni mwanamuziki ambaye Diamond anajisifia mafanikio yake akiwa ameshinda tuzo kama Zikomo (Zambia), Afrimma (Marekani), EAEA (Kenya), BET (Marekani), DIAFA (Dubai), TMA (Tanzania) na kadhalika.

Ndiye msanii wa kwanza Afrika Mashariki kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 100 Boomplay, pia akiwa msanii wa tatu kutazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 1 YouTube baada ya Diamond na Harmonize. 

Na ukubwa wa muziki wake ndio ulimuwezesha Rayvanny kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza katika jukwaa la MTV EMAs, hafla iliyofanyika Novemba 2021 huko Budapest nchini Hungary.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *