Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefichua kuwa vurugu za uchaguzi  wa Oktoba 29 ziliratibiwa na watu wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuibomoa serikali, na kuzionya vikali taasisi za dini.

Rais Samia amesema hayo leo katika hotuba yake na wazee yenye ujumbe mzito wa kiusalama.

Ameeleza kuwa baadhi ya wahusika wamekuwa wakituma salamu serikalini wakitoa masharti ya kuzungumza, lakini akasisitiza kuwa serikali haitalazimishwa wala kupewa masharti na mtu yeyote. “Serikali hii haiwezi kuamrishwa. Sisi ni nchi huru,” amesema.

Rais wa Tanzania amesema pia kuwa wapo wanaoishinikiza serikali “imuachie mtu fulani” kama sharti la maridhiano, jambo alilokataa akisema maridhiano hayataongozwa kwa mashinikizo kutoka nje.

 Ameongeza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda uchaguzi kwa asilimia 97, na kwamba wanaouliza kwa nini asilimia hiyo ni kubwa “hawakuwepo kwenye uchaguzi,” hivyo hawapaswi kutilia shaka maamuzi ya waliojitokeza kupiga kura.

Rais Samia Suluhu Hassan amezionya taasisi za dini ambazo, kwa namna moja au nyingine, amesema zimejiingiza kwenye mkumbo wa mijadala na matamko yanayochochea mgawanyiko nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Tanzania haina dini rasmi, lakini wananchi wake wana dini mbalimbali, na hakuna dhehebu lililopewa mamlaka ya kuyatamka au kuyazidi madhehebu mengine kisheria.

Akilitaja moja kwa moja Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Rais Samia alisema limekuwa likitoa matamko mara kwa mara, ikiwemo manane yaliyotolewa katika kipindi kifupi. Hata hivyo, amesema hata ndani ya TEC kuna viongozi wanaopinga matamko hayo wakiyaita batili, jambo analosema linaonesha kuwa msimamo huo si wa taasisi nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *